• HABARI MPYA

  Friday, April 05, 2024

  YANGA SC YATUPWA NJE KWA MATUTA AFRIKA KUSINI


  MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC wametupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria, Afrika Kusini.
  Katika mchezo huo wa marudiano wa Robo Fainali, Refa Dahane Beida wa Mauritania alilazimika kutumia Teknolojia ya VAR dakika ya 58 kuamua juu ya shuti la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mburkinabe, Stephane Aziz Ki lililoonekana kudundia ndani ya mstari wa lango si bao.
  Katika mikwaju ya penalti waliofunga za Mamelodi Sundowns ni viungo Mchile, Marcelo Allende, Mbrazil Lucas Ribeiro Costa na mzawa, Neo Maema wakati ya nyota kutoka Uruguay, Leandro Sirino iliokolewa na kipa Mmali, Djigui Diarra wa Yanga.
  Waliofunga penalti za Yanga ni winga Mghana, Augustine Okrah na mshambuliaji wa Ivory Coast, Joseph Guédé Gnadou huku Aziz Ki na mabeki Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wakikosa.
  Ikumbukwe mechi ya kwanza ya Robó Fainali Jumamosi iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana pia Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Sasa Mamelodi Sundowns itakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast zinazorudiana kesho baada ya sare ya 0-0 pia kwenye mechi ya kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YATUPWA NJE KWA MATUTA AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top