• HABARI MPYA

  Monday, April 15, 2024

  YANGA YASEMA INAWAHESHIMU SIMBA NI TIMU TISHIO KWENYE MBIO ZA UBINGWA


  KLABU ya Yanga imesema inawaheshimu watani wao, Simba SC kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Jumamosi kuanzia Saa 11:00 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema leo, Afisa Habari wa Yanga SC, Ally Shaaban Kamwe amesema kwamba wanaamini Simba ni timu tishio na iliyo kwenye mbio za ubingwa.
  "Kuelekea mchezo wetu wa Derby ya Kariakoo Jumamosi, sisi Young Africans SC hatuiangalii Simba kama nyie wengine mnavyoiangalia, sisi tunaingalia Simba kama timu Tishio na tunayowania nayo Ubingwa,".
  "Ni timu yenye wachezaji wazoefu na Viongozi wazuri na ndiyo maana sisi kama Young Africans SC hatuendi kwenye Derby kwa kuwaangalia Simba kama ambavyo waandishi na watu wengine wanavyoiangalia." amesema Kamwe.
  Aidha, Afisa Habari huyo amesema kwamba mchezo wameamua kuwakabidhi wazee wa klabu hiyo na wameupa jina '𝐖azee 𝐃ay' kwa heshima ya wazee wa Yanga na amewaomba wafanye dua za kutosha ili timu ishinde.
  "Sisi kama Young Africans tumeamua mchezo huu wa Jumamosi tuwakabidhi Wazee wetu, huu mchezo wa Derby wa Jumamosi ni 𝐖𝐀𝐙𝐄𝐄 𝐃𝐀𝐘 (𝐦𝐚𝐩𝐢𝐠𝐨 𝐲𝐚 𝐤𝐢𝐮𝐭𝐮 𝐮𝐳𝐢𝐦𝐚) Wazee wa Yanga wote hii mechi ni ya kwenu, tukifungwa ni nyie. Tunaomba mkatuheshimishe wazee wetu, mje kwa wingi Benjamin Mkapa lakini tunaamini pia kupitia Dua zenu tutafanya vizuri," amesema Kamwe.
  Katika hatua nyingine Kamwe ametaja viingilio vya mchezo huo ambavyo ni Sh.50,000 kwa VIP A, 30,000 VIP B, 20,000 VIP C, 10,000 viti vya Rangi ya Chungwa na 5,000 kwa Mzunguko. Hata hivyo, tayari Yanga imesema tiketi za VIP A zimekwisha. 
  Ikumbukwe mechi ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu baina ya mamba hiyo, Yanga iliibuka na ushindi wa 5-1 Novemba 5, mwaka jana hapo hapo Uwanja w Benjamn Mkapa.
  Siku hiyo mabao ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda dakika ya tatu na viungo, Mkongo Maxi Mpia Nzengeli, mawili dakika ya 64 na 77, Mburkinabe Stephane Aziz Ki dakika ya 73 na Muivory Coast Pacome Zouazoua dakika ya 87 kwa penalti.
  Refa Ahmad Arajiga wa Manyara alitoa adhabu ya penalti baada ya beki Mkongo, Henock Inonga Baka ‘Varane’ kumchezea rafu Nzengeli kwenye boksi na bao pekee la Simba lilifungwa na Kibu Dennis Prosper dakika ya tisa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YASEMA INAWAHESHIMU SIMBA NI TIMU TISHIO KWENYE MBIO ZA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top