• HABARI MPYA

  Sunday, April 21, 2024

  ONANA AOKOA PENALTI KUIPELEKA MAN UNITED FAINALI KOMBE LA FA


  TIMU ya Manchester United imefanikiwa kwenda Fainali ya Kombe la FA England baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Coventry City kufuatia sare ya mabao 3-3 leo Uwanja wa Wembley Jijini London.
  Hadi mapumziko, Manchester United walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na kiungo Mscotland Scott McTominay dakika ya 23 na beki Muingereza Harry Maguire dakika ya 45 na dakika nane baada ya kuanza kipindi cha pili kiungo Mreno Bruno Fernandes akafunga la tatu dakika ya 58.
  Coventry City wakasawazisha Mabao yote kupitia kwa mshambuliaji Ellis Simms dakika ya 71, kiungo Callum O'Hare dakika ya 79 na mshambuliaji Mmarekani, Haji Amir Wright dakika ya 90'+5.
  Na kwenye mikwaju ya penalti waliofunga za Manchester United ni Diogo Dalot, Christian Eriksen, Bruno Fernandes na Rasmus Højlund baada ya Casemiro kukosa ya kwanza.
  Waliofunga penalti za Coventry City ni Haji Amir Wright na Victor Torp, wakati mkwaju wa Callum O'Hare uliokolewa na kipa Mcameroon wa Man United, Andre Onana na wa Benjamin Sheaf ukapaa juu.
  Sasa Manchester United itakutana na mahasimu wao wa Jiji, Manchester City katika Fainali Mei 25 hapo hapo Wembley. Man City iliitoa Chelsea jana kwa kuichapa 1-0 bao pekee la Bernardo Silva  dakika ya 84.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ONANA AOKOA PENALTI KUIPELEKA MAN UNITED FAINALI KOMBE LA FA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top