• HABARI MPYA

  Thursday, December 11, 2014

  YANGA SC WAMPA MLIBERIA JEZI YA OKWI, AANZA MAZOEZI LEO KWA AJILI YA MTANI JEMBE

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  JEZI aliyokuwa anavaa Mganda Emmanuel Anold Okwi wakati yupo Yanga SC, leo amekabidhiwa mshambuliaji mpya, Kpah Sean Sherman kutoka Liberia.  
  Okwi alirejea Simba SC Agosti, baada ya kuichezea Yanga SC tangu Desemba- na japokuwa alikuwa hajamaliza Mkataba, lakini mgogoro baina yake na klabu hiyo ulimfungulia milango ya kutoka.
  Na baada ya kufuzu vipimo vya afya leo, Sherman alikwenda Uwanja wa Boko Veterani kuanza mazoezi na kikosi cha Yanga SC, kinachojiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya mahasimu Simba SC. 
  Kpah Sean Sherman akiwa mazoezini Yanga SC na jezi namba 25, ambayo alikuwa anavaa Okwi alipkuwa timu hiyo

  Sherman anatarajiwa kusaini Mkataba wa mwaka mmoja Yanga SC, baada ya awali kuwa amefikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo akiwa Cyprus.
  Kwa pamoja, Yanga SC na mchezaji huyo wana matumaini makubwa mambo yatakwenda vizuri na watafunga ndoa ya mwaka mmoja.
  Sherman mwenye umri wa miaka 22 ametua Yanga SC akitokea klabu ya Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini, ambako analazimika kuvunja Mkataba wake uliobakiza miezi minne.
  Emmanuel Okwi akiichezea Yanga SC dhidi ya Al Ahly mapema mwaka huu

  Alianza kuichezea Cetinkaya mwaka 2012, akitokea Duzkaya SK aliyoanza kuichezea mwaka 2010, akitokea Barrack YC ya nyumbani kwao, Liberia ambayo alianza kuichezea mwaka 2009.
  Sherman akifanikiwa kusaini Yanga SC, atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa dirisha la dogo baada ya kiungo mkabaji Mbrazil, Emerson de Oliviera Roque na mshambuliaji mzalendo, Danny Mrwanda aliyekuwa anacheza Vietnam.
  Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Yanga SC kama itamsajili Sherman mkali wa mabao katika Ligi ya Cyprus Kaskazini, italazimika kukata mchezaji mmoja wa kigeni ili ikidhi kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotaka wageni watano tu.
  Bila ya Sherman, tayari Yanga SC inao Wabrazil Emerson, Andrey Coutinho, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite na Mganda Hamisi Kiiza.  
  Aidha, Sherman akisajiliwa Yanga SC atakuwa Mliberia wa pili kucheza Tanzania, baada ya William Fahnbullar aliyewika Simba SC kuanzia 1997 hadi 1999 alipohamia Kajumulo WS kabla ya kutimkia Ulaya.
  Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Leonardo Leiva akimpa mazoezi Kpah Sean Sherman  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WAMPA MLIBERIA JEZI YA OKWI, AANZA MAZOEZI LEO KWA AJILI YA MTANI JEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top