• HABARI MPYA

  Sunday, December 21, 2014

  UMONY AWAADHIBU AZAM FC WAKILALA 2-0 KWA KCCA

  Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
  MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC, Brian Umony leo ameiadhibu timu yake hiyo akiichezea KCCA ya kwao, Uganda katika mchezo wa kirafiki.
  KCCA imeshinda 2-0 dhidi ya mabingwa wa Tanzania Bara Uwanja wa Lugogo mjini Kampala na Umony aliyeichezea Azam FC kwa misimu miwili iliyopita amefunga bao moja, lingine likifungwa na Herman Wasswa.
  Brian Umony aliifungia mabao 10 katika mechi 33 ndani ya misimu miwili Azam FC, ambayo muda mwingi alikuwa nje kwa majeruhi. 
  Brian Umony aliichezea Azam FC mechi 33 na kuifungia mabao 10 ndani ya misimu miwili

  Aliwaaga Azam FC kwa bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu msimu uliopita Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mchezo wa leo ulikuwa wa mwisho katika ziara ya kambi ya takriban siku 10 ya Azam FC nchini Uganda, ikishinda mechi moja na kufungwa tatu.
  Awali Azam FC ilifungwa mara mbili mfululizo 3-2 na SC Villa na 1-0 na URA kabla ya jana kushinda 3-0 dhidi ya Vipers FC jana.
  Azam FC ilikwenda Uganda kwa maandalizi ya Ligi Kuu ambayo ilisimama kwa takriban mwezi mmoja na itarejea wiki ijayo, mabingwa hao watetezi wakicheza na Yanga SC katika mzunguko wa nane.
  Kikosi cha Azam FC, chini ya kocha Mkuu Mcameroon, Joseph Marius Omog na Msaidizi wake, Mganda George ‘Best’ Nsimbe kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho kuendelea na maandalizi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UMONY AWAADHIBU AZAM FC WAKILALA 2-0 KWA KCCA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top