• HABARI MPYA

  Thursday, December 11, 2014

  SHERMAN AFUZU VIPIMO VYA AFYA YANGA SC

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Liberia, Kpah Sean Sherman amefuzu vipimo vya afya na sasa yuko kwenye majadiliano ya kimkataba na uongozi wa klabu ya Yanga SC.
  Sherman anatarajiwa kusaini Mkataba wa kujiunga na klabu ya Yanga SC, baada ya awali kuwa amefikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo akiwa Cyprus.
  Kwa pamoja, Yanga SC na mchezaji huyo wana matumaini makubwa mambo yatakwenda vizuri na watafunga ndoa ya mwaka mmoja.
  Na iwapo zoezi la Mkataba litamalizika mapema, Sherman anaweza kuingia kambini leo katika hoteli ya Landmark, Mbezi Beach, Dar es Salaam.
  Sherman akifanyiwa vipimo vya afya leo Dar es Salaam
  Daktari wa Yanga SC, Sufiani Juma aliongoza zoezi hilo
  Kpah Sean Sherman baada ya kufanyiwa vipimo

  Dk Gilbert Kigadye (kulia) akiyakagua maungo ya mchezaji huyo wakati wa kumpima kama hana majeruhi

  Yanga SC kwa sasa ipo kambini katika hoteli ya Landmark, eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam ikijiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe 2 Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Sherman anatarajiwa kucheza keshokutwa. 
  Sherman mwenye umri wa miaka 22 ametua Yanga SC akitokea klabu ya Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini, ambako analazimika kuvunja Mkataba wake uliobakiza miezi minne.
  Alianza kuichezea Cetinkaya mwaka 2012, akitokea Duzkaya SK aliyoanza kuichezea mwaka 
  2010, akitokea Barrack YC ya nyumbani kwao, Liberia ambayo alianza kuichezea mwaka 2009.
  Sherman akifanikiwa kusaini Yanga SC, atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa dirisha la dogo baada ya kiungo mkabaji Mbrazil, Emerson de Oliviera Roque na mshambuliaji mzalendo, Danny Mrwanda aliyekuwa anacheza Vietnam.
  Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Yanga SC kama itamsajili Sherman mkali wa mabao katika Ligi ya Cyprus Kaskazini, italazimika kukata mchezaji mmoja wa kigeni ili ikidhi kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotaka wageni watano tu.
  Bila ya Sherman, tayari Yanga SC inao Wabrazil Emerson, Andrey Coutinho, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite na Mganda Hamisi Kiiza.  
  Aidha, Sherman akisajiliwa Yanga SC atakuwa Mliberia wa pili kucheza Tanzania, baada ya William Fahnbullar aliyewika Simba SC kuanzia 1997 hadi 1999 alipohamia Kajumulo WS kabla ya kutimkia Ulaya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHERMAN AFUZU VIPIMO VYA AFYA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top