• HABARI MPYA

  Monday, December 29, 2014

  CHONDE CHONDE BENDI ZETU, UZINDUZI WA ALBAM SIO NYWELE

  Nywele bwana sijui kama kuna mtu hajajaaliwa kuwa nazo, hata uwe na upara vipi lakini utakuwa nazo tu japo kidogo.
  Na hata kama yupo mwenye kipara kichwa kizima basi atakuwa na japo ndevu au jamii nyingine ya nywele katika sehemu mbali mbali za mwili wake.
  Wapo wanaochukulia kuzindua albam au bendi ni jambo la lazima kama nywele ziotavyo miilini mwetu, wanalifanya ni jambo rahisi mithili ya nywele – unazikata leo, keshokutwa zinaanza kuchomoza tena.
  Wiki iliyoipita niliandika juu ya namna baadhi ya mikakati na harakati za muziki wa dansi na taarab zinavyofanana na hekaya za Pwagu na Pwaguzi, nikaonekana msaliti - mtu mmoja akaniambia sijui muziki na kunishauri mambo ya muziki niwaachie wanamuziki wenyewe.

  Ni kweli sijui muziki, lakini kwa bahati mbaya au nzuri wanamuziki wanaandaa kazi zao huku wakijua wazi kuwa wateja wao wakubwa ni sisi tusiojua muziki, sisi ndio tuko wengi kuliko wanaojua muziki, hivyo tunastahili heshima yetu, maoni yetu ni muhimu sana kwao.
  Naomba nitaje maonyesho matatu yaliyofanyika Travertine Hotel kama sehemu ya mifano mizuri ya kusherehesha nilichokiandika wiki iliyopita: Ijumaa ya tarehe 19 mwezi huu, Five Stars walizindua albam mpya “Kichambo Kinakuhusu” onyesho ambalo halikufanikiwa, kwa hesabu za haraka haraka unapata jibu kuwa kilichovunwa pale ni HASARA.
  Disemba 21, hapohapo Travertine, Jahazi Modern Taarab wakafanya onyesho maalumu la miaka 8 ya bendi yao, onyesho likafanikiwa, FAIDA ilikuwa inajionyesha wazi.
  Disemba 26, G Five Modern Taarab wakazindua albam tatu kwa mpigo pamoja na kuzindua rasmi bendi yao, onyesho likafeli, ilikuwa zaidi ya HASARA. Hayo ndio matatizo ya kugonganisha show kubwa ndani ya ukumbi mmoja katika siku zinazokaribiana, ni lazima mnyonge aumie.
  G Five Modern Taarab walifanya kila kitu kizuri kilichohitajika, kuanzia matangazo hadi wasindikizaji lakini walifeli kwenye baadhi ya mambo ikiwemo tarehe na ukumbi.
  Kiukweli kabisa, G Five  ilishazinduliwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita pale Equator Grill na kwa zaidi ya miezi mitatu limekuwa na monyesho ya moja kwa moja kila wiki ndani ya Flamingo Bar Magomeni Mwembechai, hatua chache kutoka Travetine Hotel, hivyo kusema bendi ilikuwa inazinduliwa rasmi ilikuwa ni kosa la kiufundi.
  G Five ikasema inazindua albam tatu kwa mpigo ikiwemo hadi albam ya kwanza iliyoziduliwa na bendi pale Equator Grill, albam ambazo hazina video hata moja, albam ambazo wasanii wake wengine walioshiriki wameshahama, likawa kosa lingine la kiufundi.
  Mizozo iliyotokea baina ya G Five na bendi zilizosindikiza uzinduzi huo (Extra Bongo na East African Melody) hadi kugomea kendelea kutumbuiza, pia kutokuwepo kwa mauzo ya CD za japo albam moja kati ya hizo tatu zilizozinduliwa, ni mambo yaliyoongeza idadi ya makosa ya kiufundi. 
  Ndio maana nasema uzinduzi si nywele, uzinduzi si jambo la lazima, zipo bendi nyingi zinaendelea na maisha bila hata ya kuzinduliwa rasmi, kama unaweza kupitisha mwaka mzima bila kuzindua albam huku nyimbo zenyewe zikizidi kufifia kutokana na mfumuko wa nyimbo mpya, basi hakuna haja ya kuifanyia uzinduzi.
  Albam inatakiwa izinduliwe ikiwa bado haijapoa lakini iwe na angalau wimbo mmoja unaofanya vizuri sana kwenye TV na radioni kwa wakati husika kinyume na hapo uchune tu.
  Mwisho nawapongeza G Five kwa maandalizi ya kishindo ya onyesho hilo, matangazo ya vitambaa na makaratasi (banners, posters na vipeperushi) yalizagaa kila kona ya Dar es Salaam, radioni nako matangazo yalisikika vizuri, tumieni mapungufu yaliyojitokeza kujipanga na maonyesho yenu maalum yajayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHONDE CHONDE BENDI ZETU, UZINDUZI WA ALBAM SIO NYWELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top