• HABARI MPYA

    Tuesday, December 30, 2014

    BRANDTS ALIYEFUKUZWA YANGA SC SASA ANAFUNDISHA KLABU YA LIGI KUU UHOLANZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA kocha wa Yanga SC, Mholanzi Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts sasa anafundisha FC Dordrecht ya Ligi Kuu ya kwao, Uholanzi maarufu kama Eredivisie. 
    Hiyo inakuwa timu ya kwanza Brandts kufundisha baada ya kufukuzwa Yanga SC Desemba 25, mwaka jana kufuatia kufungwa na mahasimu Simba SC mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
    Brandts aliyemrithi Mbelgiji, Tom Saintfiet Oktoba 2012, alifukuzwa Yanga SC, baada ya kuiongoza timu hiyo katika mechi 50, akiiwezesha kushinda mechi 29, sare 13 na kufungwa nane.
    Kocha wa zamani wa Yanga SC, Ernie Brandts sasa anafundisha Ligi Kuu Uholanzi

    Brandts aliipa Yanga SC taji moja la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 na hadi anafukuzwa msimu uliopita aliiacha timu hiyo inaongoza Ligi Kuu baada ya mzunguko wa kwanza.  
    Mwisho wa msimu, Yanga SC ikiwa chini ya kocha mpya, Mholanzi pia, Hans van der Pluijm iliambulia nafasi ya pili nyuma ya Azam FC walioibuka mabingwa.
    Mtaalamu huyo, aliyezaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, Brandts ni kati ya makocha wachache wa kiwango juu kufanya kazi Tanzania.
    Ni beki wa zamani wa klabu za PSV Eindhoven, Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap zote za kwao Uholanzi.
    Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978. 
    Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
    Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
    Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu Eredivisie, ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
    Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako alifanya kazi hadi mwaka 2012 alipohamia Yanga SC.
    Kwa sasa Yanga SC inafundishwa na Pluijm, aliyerejeshwa mwezi huu kuchukua nafasi ya Mbrazik, Marcio Maximo ambaye naye amefutwa kazi baada ya miezi sita, kufuatia kufungwa na Simba SC 2-0 katika Nani Mtani Jembe.
    Awali, Pluijm alifanya kazi kwa nusu ya mwisho ya msimu Yanga SC, kabla ya kuondoka mwenyewe baada ya kupata kazi Uarabuni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BRANDTS ALIYEFUKUZWA YANGA SC SASA ANAFUNDISHA KLABU YA LIGI KUU UHOLANZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top