• HABARI MPYA

  Sunday, December 28, 2014

  PHIRI ATAONDOKA, MATATIZO HAYATAKWISHA SIMBA SC, UJUAJI UMEZIDI!

  KINACHOENDELEA kwa sasa ni mjadala kuhusu uwezo wa kocha Patrick Phiri, viongozi wengi wa Simba SC wanaamini Mzambia huyo uwezo wake umekwisha.
  Wanasema amechoka, lakini tu wanahofia kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi kwa sasa, wanaweza wakatoa nafuu, wakaingiza taaban.
  Akiwa ana umri wa miaka 58, Phiri anazidiwa miaka mitano na kocha wa Manchester United, Aloysius Paulus Maria van Gaal, mwenye umri wa miaka 63. 
  Najiuliza Phiri kachokaje? Bado ukienda kwenye mazoezi ya Simba SC kazi anayoifanya, namna anavyoongoza mazoezi kwa nadharia na vitendo, hafanani na mtu aliyechoka. 
  Makocha wanaajiriwa ili wafukuzwe, hilo naafiki na kuna uwezekano kwa mara ya kwanza safari hii Phiri atafukuzwa Simba SC, iwapo mwenendo hautobadilika. 

  Kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kusimama, uongozi wa Simba SC ulimpa mechi mbili kocha Phiri baada ya sare tano mfululizo timu ifanye vizuri, vinginevyo itavunja naye Mkataba.
  Bahati nzuri kwake kocha huyo mpole Mzambia, akavuna pointi nne kwenye mechi hizo, akitoa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar na kushinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting, hivyo akanusurika na kubaki kazini.
  Wakati wa mapumziko, Phiri alichelewa kwenda nyumbani Zambia na akawahi kurudi kazini, ili kutengeneza timu. Katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Phiri akaiwezesha Simba SC kushinda 2-0 dhidi ya Yanga SC.
  Lakini katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu juzi, akafungwa 1-0 na Kagera Sugar na baada ya hapo, watu wawili wakawa wanatajwa kama sababu ya kipigo hicho.
  Kipa Ivo Mapunda aliyefungwa bao rahisi kutokana na kushindwa kuokoa mpira wa kurushwa na kocha Phiri. Naamini, iwapo Simba SC haitapata matokeo mazuri katika mechi zake mbili zijazo, dhidi ya Mgambo JKT Tanga na Mbeya City, Phiri ataondoka.
  Ataondoka tu, kwa sababu viongozi wetu hupenda kila siku kujikosha mbele ya wanachama na wapenzi wa klabu kwa kuchukua hatua katika staili maarufu za ‘kutoana kafara’.
  Akae akijua Phiri ndiye ‘Kafara’ lifuatalo Simba SC kwa matokeo mabaya. Na kwa kuzingatia kwamba hizo ni mechi ngumu kihistoria kwa Simba SC, maana yake Phiri sasa anachungulia mlango wa kutokea Msimbazi.
  Simba SC inapokwenda kucheza na Mgambo pale Tanga, huwa wanakiona cha moto na katika misimu miwili ya timu hiyo kuwa Ligi Kuu Wekundu wa Msimbazi wamewahi kuvuna pointi moja tu, tena msimu wa kwanza. 
  Mbeya City wapo katika msimu wa pili kwenye Ligi Kuu, lakini ni timu imara ambayo japokuwa msimu huu imeanza kwa kusuasua, inaweza kufanya lolote kwa Simba SC.
  Unaweza kuona kabisa huwezi kuingia kwenye michezo migumu ya aina hii ukiwa umemuwekea mtego kocha kwamba asipopata matokeo mazuri anafukuzwa. Hizo ni mechi ambazo lolote linaweza kutokea na maisha yakaendelea.
  Simba SC imekuwa katika misimu miwili mibaya iliyopita na huu unaelekea kuwa msimu mwingine wa tatu mbovu kwao, chini ya uongozi mpya wa Rais, Evans Aveva.
  Kusema chochote kuhusu uongozi wa Aveva kwa sasa ni mapema sana, lakini unaweza kuzungumzia mwenendo wa timu katika kipindi japo cha miaka mitatu iliyopita.
  Aveva anatoka kundi la Friends Of Simba, ambalo wakati wote limekuwa bega kwa bega na timu, chini ya viongozi mbalimbali, hadi mwaka huu walipoamua kuchukua timu wao wenyewe.
  Mawazo ya FOS ndiyo yamekuwa yakiiongoza Simba SC kwa miaka kadhaa sasa, tangu Hassan Daalal Mwenyekiti na hata wakati wa Alhaj Ismail Aden Rage pia, ingawa baadaye walitibuana.
  Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ yeye si Friends Of Simba, ila yupo karibu nao ingawa ‘kihivyo hivyo’, naye amekuwa karibu na timu miaka zaidi ya mitano sasa.
  Unaweza kuona kwamba, japo wameingia madarakani katikati ya mwaka, lakini Aveva na Kaburu wamekuwa wakifanya kazi Simba SC kwa miaka.
  Katika siku za mwanzoni za uongozi huu, changamoto kubwa ilikuwa ni mshikamano baina ya F.O.S. na Kaburu, lakini dalili zinaonyesha sasa hilo limepatiwa ufumbuzi.   
  Changamoto kubwa ambazo zinaikabili Simba SC kwa sasa ni mbili; kwanza ni ujuaji. F.O.S. ni wajuaji, Kaburu mjuaji na ukienda kwa Rais wa klabu, Aveva huwa ni mzito kuamua kwa sababu ni mpole, asiyependa lawama na mbaya zaidi amezungukwa na marafiki wa siku nyingi.
  Mambo mengi Simba SC yanafanyika unashindwa kuelewa haya ni mawazo ya watu makini kweli? Kosa kubwa lilifanyika Agosti mwaka huu, kumfukuza kocha Zdravko Logarusic wiki mbili baada ya kumpa Mkataba mpya, kisa tu kufungwa na ZESCO United 3-0. Niliandika mapema, kosa lile litaigharimu SImba SC katika msimu na hicho ndicho kinachoendelea kwa sasa.
  Tatizo moja, Simba SC husahau matatizo yao baada ya kuifunga Yanga SC, na ndiyo maana miaka inakatika ugonjwa unazidi kuwa sugu.
  Simba SC lazima ibadilike, haiwezekani kila mtu awe mjuaji na mwenye maamuzi katika timu, lazima watu wachache wapewe majukumu na wasiingiliwe.
  Hali ilivyo sasa, Simba SC inaongozwa kishabiki mno na si kitaalamu. Mambo yanaendelea uwanjani, watu wanajadili jukwaani, baadaye hayo hayo ndiyo yanakuwa maamuzi. 
  Vigumu sana kwa mwenendo huo na hata Phiri akiondoka, matatizo hayatakwisha. Heri ya Krisimasi na mwaka mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PHIRI ATAONDOKA, MATATIZO HAYATAKWISHA SIMBA SC, UJUAJI UMEZIDI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top