• HABARI MPYA

    Wednesday, December 24, 2014

    KOMBE LA TAIFA SOKA WANAWAKE KUANZA JANUARI MOSI

    Na Boniface Wambura, DAR ES SALAAM
    MICHUANO ya Taifa ya soka ya wanawake (Taifa Cup Wanawake) yanazinduliwa rasmi Januari Mosi mwakani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa mechi kati ya wenyeji Mwanza na Mara.
    Mechi hiyo itakayoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Azam itachezwa kuanzia saa 10 jioni. Mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Proin yatachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini katika hatua ya kwanza.
    Januari 10 mwakani ndipo zitachezwa mechi kwa mikoa yote ambapo Geita itakuwa mwenyeji wa Kagera (Uwanja wa Geita), Tabora vs Kigoma (Ali Hassan Mwinyi), Simiyu vs Shinyanga (Uwanja wa Simiyu), Arusha vs Manyara (Sheikh Kaluta Amri Abeid), na Kilimanjaro vs Tanga (Uwanja wa Ushirika).
    Mechi nyingine ni Lindi itaikaribisha Mtwara kwenye Uwanja wa Ilulu, Ruvuma vs Njombe (Uwanja wa Majimaji), Mbeya vs Iringa (Uwanja wa Sokoine), Katavi vs Rukwa (Uwanja wa Katavi), Dodoma vs Singida (Uwanja wa Jamhuri) na Pwani itakuwa mwenyeji wa Morogoro katika Uwanja wa Mabatini.
    Timu hizo zitarudiana Januari 13 mwakani, ambapo baada ya matokeo ya nyumbani na ugenini timu iliyoshinda ndiyo itakayoingia hatua inayofuata ambayo pia itashirikisha mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
    Hatua hiyo, mechi zake za kwanza zitachezwa Januari 17 mwakani wakati zile za marudiano zitafanyika Januari 21 mwakani.
    Baada ya hapo, hatua itakayofuata ni robo fainali, nusu fainali na fainali ambayo ndiyo itakayotoa bingwa wa michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
    Mdhamini atatoa jezi kwa timu zote zinazoshiriki kabla ya kuanza mashindano hayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOMBE LA TAIFA SOKA WANAWAKE KUANZA JANUARI MOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top