• HABARI MPYA

  Sunday, December 28, 2014

  HIVI NDIVYO JOHN RAPHAEL BOCCO ALIVYORUDI

  AKICHEZA mechi yake ya kwanza msimu huu, mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ leo ameendeleza desturi yake ya kuwafunga vigogo, Yanga SC.
  Bocco aliinuliwa benchi na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kipindi cha pili kwenda kuchukua nafasi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na bahati nzuri aliingia Azam FC ikipeleka shambulizi kwa wapinzani.
  Bocco alikimbia moja kwa moja kwenye boksi la Yanga SC na kukutana na krosi nzuri ya juu ya kiungo Himid Mao na kuiunganishia nyavuni kwa kichwa dakika ya 65.
  John Bocco wa pili kulia akipongezwa na wenzake baada ya kufunga
  Bocco akipambana na beki wa Yanga SC, Kevin Yondan


  Lilikuwa bao muhimu, ambalo liliinusuru Azam FC kupoteza mechi dhidi ya timu ambayo wanachuana nayo vikali katika mbio za ubingwa.
  Bao ambalo bila shaka lilipokewa kwa shangwe si tu na mashabiki wa Azam FC, bali hata benchi la ufundi, wachezaji wenzake, viongozi na wamiliki wa timu hiyo, kampuni ya Said Salim Bakhresa.
  Bocco aliumia Agosti mwaka huu kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na tangu hapo hajagusa mpira hadi leo akicheza kwa mara ya kwanza.
  Na amerudi vizuri akiisaidia timu yake kutopoteza mechi, huku akiendeleza rekodi yake ya kuwafunga Yanga SC.  Hivyo ndivyo John Raphael Bocco ukipenda muite Adebayor alivyorudi kutoka kwenye maumivu ya tangu Agosti.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HIVI NDIVYO JOHN RAPHAEL BOCCO ALIVYORUDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top