• HABARI MPYA

    Sunday, June 28, 2026

    WACHEZAJI WA YANGA SC WAZIDI KUING’ARISHA TANZANIA ‘DUNIANI’


    MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga SC, Fiston Kalala Mayele jana ameweka rekodi mbili kwa jina la Tanzania kwenye Fainali za Kombe la Dunia akiwa na timu yake ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Mayele aliyewahi kuchezea klabu ya Yanga kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 alitokea benchi dakika ya 51 kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa Real Betis ya Hispania, Cédric Bakambu kucheza mechi yake ya kwanza ya Fainali za Kombe la Dunia.
    Mayele anayechezea Pyramids FC ya Misri kwa sasa akaifungia DRC bao la pili na la ushindi dakika ya 78, kabla ya mshambuliaji, Yoane Wissa kufunga la tatu dakika ya 90’+1 katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Uzbekistan kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi K Alfajiri ya leo Uwanja wa Mercedes-Benz Jijini Atlanta, Georgia, Marekani.
    Yoane Wissa mzaliwa wa Ufaransa anayechezea klabu ya Newcastle United ya England awali aliifungia DRC bao la kusawazisha dakika ya 68 kwa penalti kufuatia mshambuliaji wa İstanbul Başakşehir ya Uturuki, Eldor Azamat oʻgʻli Shomurodov kuanza kuifungia Uzbekistan dakika ya 10. 
    Mayele anaweka rekodi mbili kwa jina la Tanzania; Moja; mchezaji wa kwanza kucheza timu ya Tanzania kucheza Fainali za Dunia na Pili; Mchezaji wa kwanza kucheza timu ya Tanzania kufunga bao kwenye Fainali za Dunia.
    Huo ni mwendelezo wa rekodi nzuri za wachezaji waliowahi kucheza Yanga SC katika medani ya Kimataifa – kwani, Mkongo mwingine, Shabani Christophe Nonda ‘Papi’ baada ya kuwatumikia wana Jangwani mwaka 1994, alikwenda kuweka rekodi kadhaa Ulaya.

    Rekodi hizo mchezaji wa kwanza kucheza Tanzania kucheza Ligi Kuu za Uswisi, Ufaransa, Italia na England na kuwa mchezaji wa kwanza na pekee hadi sasa kuwahi kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2003-2004 akiwa na AS Monaco ya Ufaransa ambayo ilifungwa 3-0 FC Porto ya Ureno iliyokuwa chini ya kocha Jose Mourinho.
    Awali, kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Sunday Ramadhan Manara aliyecheza Yanga kuanzia mwaka 1971 hadi 1975 aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza Ulaya aliposajiliwa na Heracles Almelo ya Ligi Kuu ya Uholanzi mwaka 1977.
    Akaweka pia rekodi za kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza Ligi Kuu ya Marekani katika klabu ya New York Eagles kabla ya kwenda Austria kuchezea FC St. Veit na Falme za Kiarabu (UAE) kuchezea Al Nasr – kote huko Manara alifungua milango kama Mtanzania wa kwanza kufika na kucheza.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI WA YANGA SC WAZIDI KUING’ARISHA TANZANIA ‘DUNIANI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top