• HABARI MPYA

  Tuesday, December 30, 2014

  AL AHLY WAALIKWA KOMBE LA MAPINDUZI, KCCA NA ULINZI YA KENYA NAZO ZAJA

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  MABINGWA wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwaka 2014/2015 Al Ahly ya Misri, ni miongoni mwa timu mashuhuri zilizoalikwa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2015.
  Iwapo timu hiyo itaweza kushiriki, michuano hiyo inatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa zaidi kulinganisha miaka iliyopita, kutokana na umahiri wake wa kutandaza kabumbu.
  Alhy walifanikiwa kutwaa Kombe la Shirikisho katikati ya mwezi huu mjini Cairo, baada ya kuitandika Sewe SC ya Ivory Coast bao 1-0, ambayo katika mchezo wa awali mjini Abidjan, ilishinda kwa mabao 2-1, na hivyo Ahly kunufaika na bao la ugenini.
  Akizungumza na waandishi wa habari  katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Kikwajuni, Katibu wa Kamati ya michuano hiyo, Khamis Abdalla Said, amesema patashika za kuwania kombe hilo zitaanza Januari, 01, 2015.
  Alizitaja timu nyengine kutoka nje ya Zanzibar zilizoalikwa kwenye mashindano hayo, kuwa ni Yanga, Simba, Azam na Mtibwa Sugar za Tanzania Bara, Ulinzi kutoka Kenya na KCCA ya Uganda ambayo ndio bingwa wa mashindano yaliyopita.
  Mabingwa wa Kombe la Shirikisho, Al Ahly ya Misri wamealikwa Kombe la Mapinduzi

  Kwa upande wa timu za Zanzibar, Khamis alisema zitakuwa ni KMKM, Shaba, Polisi, JKU, Mtende Rangers na Mafunzo, na kuongeza kuwa uwanja wa Amaan pekee ndio utakaotumika kwa michuano hiyo.
  Kuhusu matayarisho ya michuano hiyo, Khamis alisema mbali na kukubali kusaidia huduma za maji kwa muda wote, Kampuni ya Azam pia imejitolea kuzisafirisha timu zote kutoka Tanzania Bara hadi Zanzibar pamoja na ile ya kutoka Pemba kwa wastani wa wachezaji 15 kwa kila timu.
  Alisema pia Kampuni hiyo, kupitia AZAM TV ina azma ya kuonesha michuano hiyo moja kwa moja, endapo mambo yatakwenda kama yanavyopangwa.
  Alieleza kuwa, pamoja na michuano ya mwaka huu kukosa mdhamini, Kamati yake kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inafanya kila juhudi kuona mashindano hayo yanafanikiwa kwa kiwango kikubwa.
  "Ilikuwa vigumu kuwafuata wadhamini kutokana na mazingira yaliyokuwepo katika Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kwani yalichangia baadhi ya timu kushindwa kuthibitisha ushiriki wao kwa wakati uliopangwa," alisema Khamis.
  Aliwataka viongozi, kampuni, mashirika na taasisi zitakazoguswa na michuano hiyo kujitokeza na kutuma misaada yao kwa Kamati inayohusika.
  Alisema tayari Kamati imeshafanya matayarisho yote, ikiwemo kukagua viwanja vya mazoezi, kuandaa gari za wachezaji na viongozi, huduma za chakula pamoja na kuzungumza na hoteli zitakazopokea timu shiriki.
  Aidha alivitaja viingilio katika mechi za mashindano hayo, kwamba vitakuwa kati ya shilingi 2,000 na sh. 5000 kwa jukwaa la VIP.
  Alitoa angalizo kwa watu wote ikiwemo viongozi watakaofika kuangalia michuano hiyo kuhakikisha wanakata tiketi na kuacha kutegemea bure.
  “Michuano hii haina mfadhili, uendeshaji unategema mapato ya milangoni, hivyo kila mmoja hususan viongozi wachangie kwa kukata tiketi,” alisema.
  Katika hatua nyengine, alisema matawi ya klabu mashuhuri za Simba, Yanga na Azam yaliyopo Zanzibar, yameandaliwa utaratibu kwa wapenzi wao kukaaa katika maeneo maalum, endapo watahitaji tiketi za pamoja.
  Alifahamisha kuwa mchezo wa fainali umepangwa kufanyika Januari 13, 2015 ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
  Wakati huo huo: Azam, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga zitashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika kisiwani Zanzibar kuanzia Januari 1 hadi 13 mwakani.
  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa ruhusa kwa timu hizo kucheza mashindano hayo baada ya kuhakikishiwa na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kuwa kesi iliyofunguliwa dhidi ya viongozi wake imeondolewa mahakamani.
  Kutokana na timu hizo kushiriki Kombe la Mapinduzi, mechi zao za raundi ya tisa na kumi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zitachezwa katikati ya wiki baada ya kumaliza mechi zao za michuano hiyo.
  Hivyo mechi za VPL ambazo hazitachezwa wikiendi hii ni kati ya Azam na Mtibwa Sugar, Mbeya City na Yanga, na ile kati ya Mgambo Shooting na Simba. Mechi za wikiendi ijayo zinazopisha michuano hiyo ni kati ya Kagera Sugar na Azam, Coastal Union na Yanga, Mbeya City na Simba, na Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AL AHLY WAALIKWA KOMBE LA MAPINDUZI, KCCA NA ULINZI YA KENYA NAZO ZAJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top