• HABARI MPYA

  Tuesday, December 30, 2014

  SIMBA SC NA MTIBWA SUGAR KUFUNGUA DIMBA KOMBE LA MAPINDZI ALHAMISI, AZAM NA KCC, YANGA NA SC VILLA

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  SIMBA SC na Mtibwa Sugar, keshokutwa wanatarajiwa kukata utepe wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015 uwanja wa Amaan, kuanzia saa 2:15 ukiwa mchezo wa kundi C.
  Pambano hilo linatarajiwa kuwa la marudiano kufuatia timu hizo kufungana bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
  Katibu wa Kamati ya Mashindano hayo Khamis Abdallah Said, alisema mchezo huo utatanguliwa na mwengine wa kundi hilo kati ya maafande wa Mafunzo na JKU utakaoanza saa 9:00 mchana.
  Mechi za kundi A zitaanza kwa pambano kati ya Shaba na Polisi mnamo saa 11:00 jioni.
  Khamis, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), alisema mashindano hayo sasa yatashirikisha timu za Tanzania na Uganda pekee baada ya timu ya Ulinzi ya Kenya na Al Ahly ya Misri kushindwa kuthibitisha ushiriki wao. 
  Simba SC wataanza na Mtibwa Sugar Alhamisi Kombe la Mapinduzi


  Alifahamisha kuwa nafasi moja itajazwa na Sports Club Villa ya Uganda, na nyengine itatajwa baadae lakini itakuwa kutoka Zanzibar.
  Ratiba hiyo inaonesha kuwa, Januari 2, mwakani mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Azam FC, watatiana mikonini KCC ambao ndio wanaotetea taji hilo, zikiwa kundi B.
  Mapema wakati wa alasiri, kutakuwa na mchezo mwengine wa kundi hilo, baina ya Mtende Rangers na mabingwa wa soka Zanzibar, KMKM.
  Yanga SC ambao kwa miaka miwili iliyopita hawakushiriki mashindano hayo kwa sababu mbalimbali, wataanza resi za kuwania taji hilo Januari 3, dhidi ya Sports Club Villa ya Uganda katika mchezo wa kundi A.
  Wakati wa saa 10:00 alasiri, kutakuwa na mechi ya kundi C kati ya wajenga uchumi wa Zanzibar JKU na wazalishaji sukari wa Morogoro, Mtibwa Sugar.
  Kwa jumla, timu zinazoshiriki mashindano hayo zimepangwa katika makundi matatu, ambapo kundi A linajumuisha timu za SC Villa, Yanga SC, Polisi na Shaba.
  Mabingwa wa kombe hilo KCC, Azam FC, KMKM na Mtende Rangers ziko kundi B,  huku kundi C likiundwa na wekundu wa Msimbazi Simba SC, Mtibwa Sugar, JKU na Mafunzo.
  Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya robo fainali, na timu mbili zitapatikana kutokana na washindwa waliofanya vizuri (Best Loosers).
  Fainali ya ngarambe hizo imepangwa kupigwa Januari 13, 2015.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC NA MTIBWA SUGAR KUFUNGUA DIMBA KOMBE LA MAPINDZI ALHAMISI, AZAM NA KCC, YANGA NA SC VILLA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top