• HABARI MPYA

  Sunday, December 21, 2014

  NANDWA AANZA VYEMA COASTAL UNION, AIFUMUA 3-1 KOMBAINI YA MOMBASA LEO

  Na Vincent Malouda, MOMBASA
  KOCHA mpya wa klabu ya Ligi Luu ya Vodacom Tanzania Bara, Coastal Union James Nyende Nandwa alisajili ushindi wake wa kwanza kwenye benchi la kiufundi Coastal ilipowalaza Mombasa Combined 3 – 1 kwenye mtanange wa kirafiki uliyosakatwa alasiri ya leo uwanjani Mombasa Sports Club.
  Wenyeji walifungua nyavu za wageni mnamo dakika ya 15 kupitia kwa kichwa chake Makame Salim aliyeunganisha krosi yake mshambulizi chipukizi wa klabu ya ligi kuu ya taifa la Kenya, Bandari FC, Shaban Kenga.

  Mnamo dakika ya 32, mshambulizi wa timu ya taifa la Kenya, Harambee Stars, Ramadhan Salim alizawazisha bao hilo baada ya kubadilishana pasi moja mbili na Itubu Imbem zamani akiipigia AFC Leopards, Gor Mahia na Tusker za Kenya kabla ya kuhamia Vietnam.
  Baada ya kipindi cha mapumziko, Imbem alisajili jina lake kwenye orodha ya wafungaji mnamo dakika ya 46. Mzawa huyo wa Congo alirejea tena na kuipa Coastal Union bao la tatu kupitia tuta la penalti mnamo dakika ya 73 baada ya Abdallah Hassan wa Mombasa Combined kufanya madhambi kwenye eneo hatari.
  Hii ilikuwa mechi ya pili kwa kocha Nandwa baada ya kumridhi Yusuf Chippo aliyehamia klabu ya AFC Leopards ya Kenya kama kocha msaidizi.
  Kwenye ngarambe ya kwanza, Nandwa alisajili sare tasa dhidi ya Mwadui Shinyanga siku ya alhamisi katika uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Awali, Wagosi wa Kaya waliwatembelea watoto mayatima kwenye makao yao ya Tabarak mjini Mombasa na kuwazawidi mipira miongoni mwa zawadi zingine sherehe za Krismasi zikinukia nukia.
  Klabu hiyo inatarajiwa kurejea kwao Tanga usiku huu kulingana na mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Kenya, FKF, tawi la Mombasa kusini, Evans Mwachia.
  "Wanaenda kujitayarisha kisha warejee makwao. Mechi imekuwa nzuri sana na umati wa mashabiki uliokuwa uwanjani utathibitisha hilo," Mwachia aliiambia BIN ZUBEIRY baada ya mechi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NANDWA AANZA VYEMA COASTAL UNION, AIFUMUA 3-1 KOMBAINI YA MOMBASA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top