• HABARI MPYA

    Sunday, December 28, 2014

    AZAM NA YANGA SARE 2-2 TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imegawana pointi na Azam FC baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Mabingwa wa Bara, Azam FC watamshukuru mshambuliaji wao majeruhi wa muda mrefu, John Bocco ‘Adebayor’ ambaye akicheza kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kutokea benchi, aliifungia timu hiyo bao la kusawazisha.
    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Mathew Akrama wa Mwanza, hadi mapumziko, tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1.
    Azam FC walitangulia kupata bao kupitia kwa Mrundi, Didier Kavumbangu dakika ya tano akiupitia mpira uliotemwa na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ kufuatia krosi ya mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Tchetche.
    Wafungaji wa mabao ya Yanga SC leo, Amisi Tambwe kulia na Simon Msuva
    Mfungaji wa bao la kwanza la Azam FC, Didier Kavumbangu akishangilia 

    Yanga SC wakasawazisha bao hilo dakika mbili baadaye kupitia kwa Mrundi pia, Amisi Tambwe aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Salum Telela. 
    Kwa ujumla, timu zote zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza, Yanga SC wakipitisha zaidi mipira yao pembeni na Azam FC kadhalika, ingawa wao mashambulizi yao yalikuwa makali zaidi, kwa sababu waliiteka sehemu ya katikati ya Uwanja.
    Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na Simon Msuva dakika ya 51 akimalizia krosi ya Danny Mrwanda.
    Mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyetokea benchi kipindi cha pili alikwenda kuisawazishia Azam FC dakika ya 65, akimalizia krosi ya Himid Mao.
    Beki wa Yanga SC, Kevin Yondan, akiondoka na mpira mbele ya kiungo wa Azam FC, Salum Abubakar 'Sure Boy'
    Mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche akimtoka Juma Abdul

    Kwa ujumla mchezo huo ulikuwa mkali na wa kusisimua na timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu hadi kipyenga cha mwisho.
    Matokeo haya, yanafanya timu hizo ziendelee kufungana kwa pointi 14 kila mmoja, baada ya mechi nane zikiwa nyuma ya Mtibwa Sugar inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 16.
    Vikosi vilikuwa; Yanga SC; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Edward Charles/Oscar Joshua dk46, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amisi Tambwe/Mrisho Ngassa dk75, Kpah Sherman na Danny Mrwanda/Hussein Javu dk73.
    Azam FC; Mwadini Ali, Himid Mao/David Mwantika dk89, Shomary Kapombe, Aggrey Morris, Serge Wawa, Erasto Nyoni, Mudathir Yahya, Salum Abubakar/John Bocco dk64, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche na Brian Majwega.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM NA YANGA SARE 2-2 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top