• HABARI MPYA

  Monday, December 29, 2014

  KOCHA MDACHI ATUPIWA VIRAGO KENYA BAADA YA SIKU 224 AFISINI

  Na Vincent Malouda, NAIROBI
  KOCHA wa AFC Leopards ya Kenya na Mdachi Hendrik Pietter De Jongh hatimaye ametupiwa virago baada ya kutwikwa majukumu ya kuiongoza timu hiyo siku 224 zilizopita.
  De Jongh aliingia AFC ukipenda Ingwe kwa mkataba wa mwaka mmoja tarehe 19 Mei mwaka huu kuchukuwa nafasi yake James Nandwa.
  Akiwa Leopards, kwa mechi 28 akiwa kwenye benchi la kiufundi, De Jongh alishinda mechi 15, akatoka sare mara sita na kupoteza mechi saba tu.

  Kocha Mholanzi Hendrik Pietter De Jongh amefukuzwa AFC Leopards 

  Mechi hizo zinajumuisha sita za kombe la CECAFA Nile Basin ambapo alishinda tano na kupoteza moja kwenye fainali dhidi ya Victoria University ya Uganda Juni tarehe nne.
  Hata hivyo, atasalia kipenzi cha wachache alipowaadhibu mahasimu wa Leopards, Gor Mahia 3 – 1 kwenye mechi ya ligi kuu na kisha kutoka 2 – 2 kwenye mkondo wa pili kwenye debi hilo la ‘Mashemeji’.
  Kutupiwa kwake virago kulitangazwa rasmi na mwenyekiti Allan Kasavuli kwenye mkutano wa dharura uliyofanyika Jumapili 28  jijini Nairobi.
  Kasavuli alisema watazindua benchi mpya la kiufundi, akiwemo kocha mpya mapema mwaka ujao. Tayari Leopards wamemuajiri aliyekuwa kocha wa Coastal Union Yusuf Chippo kama kocha msaidizi na Idd Mohammed Salim kama kocha wa walindamlango. Meneja wa timu anasalia Willis Wafula Waliaula, Patrick Ngusale akiwa daktari wa timu.
  Awali Leopards, ilimwachisha kazi naibu kocha Juma Abdalla na kocha wa magolikipa Washingtone Muhanji kwa kuchangia Leopards kumaliza ligi nambari sita kwa alama 41 tu, 19 nyuma ya mahasimu wao Gor Mahia waliotawazwa mabingwa.
  Katibu mkuu George Aladwa, naibu wake Profesa Asava Kadima na wanachama wa kamati ya utendaji Esther Luvembe na Steven Mugo ni miongoni mwa waliyohudhuria hafla hiyo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA MDACHI ATUPIWA VIRAGO KENYA BAADA YA SIKU 224 AFISINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top