• HABARI MPYA

  Tuesday, December 30, 2014

  NYOTA AJAX ATEMWA BAFANA KIKOSI CHA AFCON

  Na Mwandishi Wetu, JOHANNESBURG
  NYOTA wa Ajax Amsterdam, Thulani Serero ameachwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa Bafana Bafana kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika 2015, ambazo zitaanza Januari 17 hadi Februari 8.
  Serero aliitwa katika kikosi cha awali cha wachezaji 34 na alitarajiwa kujiunga na kambi fupi iliyoanza Desemba 26, hata hivyo mchezaji huyo hakutokea baada ya klabu yake, kuiomba timu ya taifa impe mapumziko licha ya kwamba aliwasili siku mbili kabla ya kambi kuanza.
  Kocha wa Bafana, Shakes Mashaba amewapa nafasi wachezaji wengi zaidi waliocheza mechi za kufuzu AFCON 2015 na kiungo Dean Furman kutoka England anatarajiwa kujiunga na kambi mwezi ujao akimaliza majukumu ya klabu.
  Thulani Serero ametemwa kikosi cha Bafana Bafana

  Mashaba ameita makipa watatu, mabeki saba, viungo tisa na washambuliaji wane na Bafana Bafana itavunja kambi kwa mapumziko mafupi na wachezaji watakutana tena ijumaa, Januari 2 kabla ya siku mbili baadaye, kucheza mechi ya kirafiki na Zambia Uwanja wa Orlando mjini Soweto. 
  Bafana Bafana itakwenda Gabon Januari 6 kwa kambi ya mwisho ambako pia itacheza mechi kadhaa za kujipima nguvu dhidi ya Cameroon mjini Libreville Januari 10 na Gabon Januari 13 au 14, kabla ya kwenda Equatorial Guinea siku inayofuata.
  Bafana Bafana itacheza mechi ya kwanza na Algeria Januari 19, ya pili na Senegal Januari 23 na ya mwisho na Ghana Januari 27, mechi zote za kundi lao wakicheza mjini Mongomo.
  Kikosi cha mwisho cha Bafana ni; Makipa; Brilliant Khuzwayo, Darren Keet na Jackson Mabokgwane, Mabeki; Siyabonga Nhlapo, Patrick Phungwayo, Anele Ngcongca, Thulani Hlatshwayo, Mulomowandau Mathoho, Rivaldo Coetzee na Thabo Matlaba, viungo; Themba Zwane, Andile Jali, Reneilwe Letsholonyane, Bongani Zungu, Thamsanqa Sangweni, Dean Furman, Thuso Phala, Mandla Masango na Oupa Manyisa na washambuliaji Bernard Parker, Tokelo Rantie, Bongani Ndulula na Sibusiso Vilakazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NYOTA AJAX ATEMWA BAFANA KIKOSI CHA AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top