• HABARI MPYA

  Wednesday, December 24, 2014

  BARUA YATUMWA KUTOKA LIBERIA KUMHALALISHA SHERMAN YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Aries FC ya Liberia imeisuta Cetinkaya ya Cyprus Kaskazini kuhusu mshambuliaji Kpah Sean Sherman.
  Cetinkaya inayocheza Birinci Lig, Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini ambao si wanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), imewasilisha malalamiko Yanga SC, wakidai Sherman ni mchezaji wao.
  Lakini Aries wamemaliza utata kwa kutuma barua, wakimruhusu Sherman kuhamia Yanga SC, baada ya awali kumpeleka kwa mkopo Cetinkaya FC.
  Barua ya Aries iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake, Augustine Davidson na nakala yake kutua katika ofisi na BIN ZUBEIRY imesema kwamba mchezaji huyo amehamishiwa Yanga SC ya Tanzania kwa Baraka za Chama cha Soka Liberia.  
  Hii ndiyo barua kutoka Liberia ikimhalalisha Sherman kupiga kazi Jangwani

  Mapema jioni ya leo, Sherman alisema yeye ni mchezaji halali wa Yanga SC na kwamba madai ya klabu ya Cetinkaya FC ni ya kupuuzwa.
  Lakini akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Sherman ambaye yupo na Yanga SC kambini Bagamoyo, amesema kwamba Cetinkaya ni waongo, kwani alikuwa klabu hiyo kwa mkopo kutoka Aries FC ya kwao Liberia.
  “Nilipokamilisha mazungumzo na Yanga SC na kuamua kuja Tanzania kucheza, niliwaaga. Hawakutaka niondoke, nikawaambia lazima niondoke kufuata maslahi mazuri,” amesema Sherman.
  “Kwa kweli sikuridhika kuendelea kucheza pale, wale hawatambuliwi FIFA, nisingeweza kuonekana popote zaidi ya kuwafurahisha watu wa pale tu, nimekuja hapa Tanzania kwa malengo,”amesema na kuongeza; “Nataka kucheza hapa nionekane nipate timu Ulaya, au Afrika Kusini,”amesema.
  Tayari Yanga SC imepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji huyo kutoka Liberia na klabu Aries imetoa barua ya kumruhsu mchezaji huyo kuendelea na maisha Tanzania.
  Sherman amesema yeye hakuwa na Mkataba na klabu ya Cetinkaya 

  Kuhusu madai kwa nini ITC itoke Liberia badala la Cyprus Kaskazini alipokuwa anacheza mchezaji huyo, Sherman anasema; “Hawakuwahi kupata ITC yangu, wale si wanachama wa FIFA, hawawezi kuwa katika mfumo wa ITC, ndiyo maana baada ya kukamilisha uhamisho Yanga, ITC imetoka Liberia ambako FIFA inatambua nilicheza mara ya mwisho,”.
  Ameongeza; “Baada ya kusikiwa wametuma barua Yanga, niliwapigia simu kuwauliza kwa nini wanataka kuniharibia, hawakuwa na majibu, lazima wawe waungwana na waheshimu nilichofanya kwao. Waniache nitafute maisha,”amesema.   
  Sherman aliwavutia mno mashabiki wa Yanga SC wakati anaichezea kwa mara ya kwanza timu hiyo Desemba 13, mwaka huu katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, licha ya kufungwa 2-0 na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BARUA YATUMWA KUTOKA LIBERIA KUMHALALISHA SHERMAN YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top