• HABARI MPYA

  Wednesday, December 24, 2014

  AZAM FC WAMEPATA MPINZANI KWELI AFRIKA, LAKINI YANGA WASHINDWE WENYEWE TU!

  RATIBA ya michuano ya soka ya klabu Afrika mwakani imetoka na kwa mara nyingine wawakilishi wa Tanzania, Azam FC na Yanga SC wamepata wapinzani tofauti.
  Mabingwa wapya wa Tanzania Bara, Azam  FC watamenyana na El Merreikh ya Sudan katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani. 
  Kwa mujibu wa ratiba ya Raundi ya Awali iliyopangwa juzi mjini Cairo, Misri mechi za kwanza zitachezwa kati ya Februari 13 na 15 wakati marudiano yatakuwa Februari 27 na Machi 1 na Azam FC wataanzia nyumbani.
  Wakifanikiwa kuwatoa Wasudan hao, Azam FC watamenyana na mshindi kati ya Lydia Ludic B.A. ya Burundi au Kabuscorp do Palanca ya Angola.

  Ikumbukwe Azam FC ilitolewa na Merreikh katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Agosti mwaka huu mjini Kigali, Rwanda kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90. 
  Baadaye Azam FC ikamchukua beki wa Merreikh, Serge Wawa Pascal raia wa Ivory Coast na ikamkosa kidogo mshambuliaji Mohamed Traore kutoka Mali- hivyo mechi baina ya timu inatarajiwa kuwa na upinzani mkali. 
  Katika Kombe la Shirikisho, Yanga SC itamenyana BDF IX ya Botswana katika hatua ya awali mwakani. 
  Kwa mujibu wa ratiba ya Raundi ya Awali iliyopangwa leo mjini Cairo, mechi za kwanza zitachezwa kati ya Februari 13 na 15 wakati marudiano yatakuwa Februari 27 na Machi 1 na Yanga SC itaanzia nyumbani dhidi ya timu ya jeshi la Botswana.
  Ikifanikiwa kuvuka mtihani huo, Yanga itamenyana na mshindi kati ya Sofapaka ya Kenya na Platinum ya Zimbabwe katika kuwania kuingia hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo.
  Mwaka huu, Yanga SC walicheza Ligi ya Mabingwa na wakatolewa hatua ya 32 Bora na Al Ahly ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 1-1 kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Yanga ilifungua ukurasa mpya mwaka huu, baada ya kufanikiwa kwa mara ya kwanza kushinda mechi dhidi ya Al Ahly na timu za Misri kwa ujumla.
  Yanga SC walipambana na unaweza kusema walikufa kiume, kwani walikutana na wapinzani shupavu ambao mwisho wa siku wamekuwa mabingwa wa Kombe la Shirikisho.
  Ahly baada ya kutolewa katika 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa mwaka huu, wakaangukia kwenye Kombe la Shirikisho ambako wamekwenda hadi kutwaa Kombe.  
  Azam FC mwaka jana waliwaangusha mno mashabiki wao na Watanzania kwa ujumla, baada ya kutolewa Raundi ya awali tu na Ferroviario de Nampula ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 wakishinda 1-0 nyumbani na kwenda kufungwa 2-0 ugenini.
  Ikumbukwe mwaka jana, Azam FC walikaribia kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa kwa mbinde na FAR Rabat ya Morocco, lakini mwaka huu walikuwa wepesi mno.
  Ukienda kwenye Ratiba ya mwaka huu, Azam FC kwa mara nyingine wamepewa mpinzani tishio wa kuanza naye, Merreikh.
  Hawa Merreikh wanapoingia kwenye michuano ya Afrika, dhamira ya kwanza ni kufika hatua ya makundi, kitu ambacho si utamaduni wetu Watanzania.
  Azam FC wamewekwa reli ngumu kupangiwa Merreikh na wanapaswa kujua wanahitaji kujiandaa vizuri kwa ajili ya mechi zote mbili, ya nyumbani na ugenini kama wanataka kuvuka hatua hiyo.
  Na bado utaona Azam FC hata ikivuka hapo, mpinzani ajaye Lydia Ludic B.A. ya Burundi au Kabuscorp do Palanca ya Angola naye ni tishio pia.
  Hii maana yake, Azam FC kama wanataka kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika wajiwekee mipango na mikakati thabiti ya kuijengea uwezo timu yao.
  Kwa Yanga SC, wamebahatika kupata wapinzani wa kawaida katika hatua mbili za awali. BDF si timu ya kutisha, hata hiyo Sofapaka au Platinum, lakini pamoja na yote, maandalizi mazuri ni muhimu.
  Yanga SC kwanza lazima wajiwekee malengo kwenye mashindano hayo, na baada ya hapo wawe na maandalizi mazuri, tena ya kisayansi kuelekea mechi zote hizo.
  Lakini wakisubiri kama ilivyo desturi yao ya maandalizi ya zimamoto, wakienda Botswana litarudi jina tu. Ila ukweli ni kwamba, baada ya droo ya CAF juzi, Azam FC wamepata mpinzani kweli, lakini Yanga SC, njia nyeupe, washindwe. wenyewe. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC WAMEPATA MPINZANI KWELI AFRIKA, LAKINI YANGA WASHINDWE WENYEWE TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top