• HABARI MPYA

    Wednesday, December 31, 2014

    KOCHA MPYA SIMBA ASEMA; “YANGA WAPO KWENYE KIGANJA CHA MKONO WANGU”

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MSERBIA Goran Kopunovic amesema kwamba anawajua sana Yanga SC na hakuja Simba SC kutalii, bali amekuja kufanya kazi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo, baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Kopunovic amesema kwamba amefurahi sana kutua Simba SC.
    “Simba SC ni klabu kubwa, nimefurahi sana kuja hapa, hii ni timu kubwa na ninataka kuleta mafanikio hapa na kuwapa furaha mashabiki,”amesema.
    Kaponovic amesema anatarajia kukutana na uongozi wa Simba SC kwa mazungumzo na kusaini Mkataba na baada ya hapo ataanza kazi rasmi na amesistiza; “Sikuja hapa kama mtalii, nimekuja kufanya kazi,”.
    Goran Kopunovic akiwa mwenye furaha baada ya kuwasili JNIA
    Hili ndilo gari lililompokea Kopunovic Uwanja wa Ndege

    Akizungumzia kuhusu wapinzani wa jadi, Yanga SC, Kopunovic amesema kwamba anawajua vizuri na anafahamu kuhusu soka ya Tanznaia kwa ujumla.
    “Nawajua Yanga SC, lakini sitapenda kuwazungumzia kwa sababu nimekuja hapa kufanya kazi ya kufundisha Simba SC. Nafahamu kuna vipaji hapa na nina taarifa za wachezaji wengi wa hapa,”amesema Mserbia huyo anayekuja kumrithi Mzambia, Patrick Phiri.
    Kopunovic anaweza kusaidiwa na mwalimu ambaye waliwahi kufanya naye kazi katika timu tofauti, Rwanda, Jean Marie Ntagwabila ambaye Simba SC imefanya naye mazungumzo.
    Kopunovic alifanya kazi kwa mafanikio nchini Rwanda akiwa na klabu ya Polisi kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Vietnam ambako pia alipata mafanikio.
    Kocha huyo anayefundisha soka maridadi ya kuburudisha, kushambulia na sifa yake kubwa ni wachezaji wake kuwa na nguvu na kasi kutokana na aina ya mazoezi anayowapa.
    Simba SC inafikia hatua ya kuachana na Phiri baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu chini yake tangu ameanza kazi Agosti mwaka huu akirithi mikoba ya Zdravko Logarusic raia wa Croatia.
    Simba SC iliachana na Logarusic kwa sababu tu ya tabia zake za kifedhuli, ambazo ilijaribu sana kumkemea, lakini hakuwa tayari kubadilika na ikaamua kumrejesha Phiri kutokana na historia yake ya kufanya kazi kwa mafanikio awali katika klabu hiyo. 
    Hata hivyo, safari hii mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa baina ya Phiri na Simba SC na ndoa yao inafikia tamati, Kopunovic akiingia kazini.
    Phiri aliiongoza Simba SC kwa mara ya mwisho Desemba 26, ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Tangu amekuja Simba SC kwa mara ya tatu Agosti mwaka huu, Phiri ameiongoza Simba SC katika mechi 22 na kushinda nane, kati ya hizo moja tu ya Ligi Kuu 1-0 dhidi ya Ruvu Shooitng na moja ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga SC 2-0, wakati amefungwa tano na kutoka sare tisa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MPYA SIMBA ASEMA; “YANGA WAPO KWENYE KIGANJA CHA MKONO WANGU” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top