• HABARI MPYA

  Tuesday, December 30, 2014

  NTAGWABILA: NIKO TAYARI KUFANYA KAZI NA GORAN SIMBA SC

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  KOCHA Jean Marie Ntagwabila amesema kwamba yuko tayari kuwa Msaidizi wa Mserbia, Goran Kopunovic katika klabu ya Simba SC.
  Akizungumza na BIN ZUBERY leo mjini Kigali, Rwanda, Ntagwabila amesema kwamba anamfahamu Kopunovic kwa sababu walifanya naye kazi Rwanda na anaheshimu uwezo wake.
  “Nipo tayari kabisa kufanya kazi chini ya Goran, ni mwalimu mzuri na tulikutana katika Ligi ya Rwanda akanifunga,”amesema Ntagwabila, ambaye ni kocha mwenye heshima kubwa Rwanda.
  Jean Marie Ntagwabila amekubali kufanya kazi chini ya Goran Simba SC

  Ntagwabila aliifanya APR iwe tishio mno kiasi cha kufikia kuifunga Zamalek ya Misri mabao 4-1 mwaka 2004 katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikitoka kufungwa 3-2 katika mchezo wa kwanza Cairo.
  APR ilisonga mbele hatua ya 16 Bora, ambako ilikwenda kutolewa kwa mbinde na Africa Sports ya Ivory Coast kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Tayari Simba SC imefikia makubaliano Kopunovic, ambaye atawasili kesho Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini Mkataba kurithi mikoba ya Mzambia, Patrick Phiri.
  Na Simba SC imezungumza na Ntagwabila aje kuwa Msaidizi wa Kopunovic- maana yake Suleiman Matola naye aliyekuwa msaidizi wa Phiri ataondolewa pia.
  Kopunovic alifanya kazi kwa mafanikio nchini Rwanda akiwa na klabu ya Polisi kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Vietnam ambako pia alifanya kazi kwa mafanikio.
  Kocha huyo anafundisha soka maridadi ya kuburudisha, kushambulia na sifa yake kubwa ni wachezaji wake kuwa na nguvu na kasi kutokana na aina ya mazoezi anayowapa.
  Simba SC inafikia hatua ya kuachana na Phiri baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu chini yake tangu ameanza kazi Agosti mwaka huu akirithi mikoba ya Zdravko Logarusic raia wa Croatia.
  Simba SC iliachana na Logarusic kwa sababu tu ya tabia zake za kifedhuli, ambazo ilijaribu sana kumkemea, lakini hakuwa tayari kubadilika na ikaamua kumrejesha Phiri kutokana na historia yake ya kufanya kazi kwa mafanikio awali katika klabu hiyo. 
  Hata hivyo, safari hii mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa baina ya Phiri na Simba SC na ndoa yao inafikia tamati, Kopunovic akiingia kazini.
  Phiri aliiongoza Simba SC kwa mara ya mwisho Desemba 26, ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Tangu amekuja Simba SC kwa mara ya tatu Agosti mwaka huu, Phiri ameiongoza Simba SC katika mechi 22 na kushinda nane, kati ya hizo moja tu ya Ligi Kuu 1-0 dhidi ya Ruvu Shooitng na moja ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga SC 2-0, wakati amefungwa tano na kutoka sare tisa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NTAGWABILA: NIKO TAYARI KUFANYA KAZI NA GORAN SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top