• HABARI MPYA

  Monday, December 22, 2014

  OKWI AREJEA LEO SIMBA SC BAADA YA KUBEBA JIKO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI tegemeo wa Simba SC, Emmanuel Okwi anatarajiwa kurejea leo kujiunga na wenzake waliopo kambini visiwani Zanzibar baada ya kuwa kwao, Uganda kwa ajili ya kuoa.
  Okwi alitarajiwa kufunga pingu za maisha na mpenzi wake mwishoni mwa wiki na baada ya hapo hatahitaji fungate, zaidi ya kuwahi kazini.
  Makamu wa Rais wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameiambia BIN ZUBEIRY mwishoni mwa wiki kwamba Okwi alikuwa ana ruhusa maalum ya kwenda kufunga ndoa kwao, na atarejea mapema mwanzoni mwa wiki.
  Emmanuel Okwi anarudi leo baada ya kufunga ndoa mwishoni mwa wiki mjini Kampala

  “Okwi amekwenda kuoa na atarudi baada ya kuoa tu na moja kwa kwa moja kwenda kuungana na wenzake kambini Zanzibar,”amesema Kaburu.
  Okwi ambaye alicheza vizuri Simba SC ikiifunga mabao 2-0 Yanga SC katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, atategemewa kuiongoza tena timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar Desemba 26, mwaka huu. 
  Okwi ni kati ya Waganda watano, wanaochezea Simba SC wengine wakiwa ni mabeki Juuko Murushid, Joseph Owino na washambuliaji Simon Sserunkuma na Dan Sserunkuma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI AREJEA LEO SIMBA SC BAADA YA KUBEBA JIKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top