• HABARI MPYA

  Sunday, December 21, 2014

  PLUIJM: NITAREJESHA RAHA NA SOKA YA KUSHAMBULIA, KUBURUDISHA YANGA SC

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema kwamba atarejesha mfumo wa uchezaji wa kushambulia na soka ya kuburudisha ndani ya timu hiyo.
  Pluijm ameyasema hayo leo asubuhi katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
  Kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana, amerejeshwa Yanga SC wiki iliyopita kuchukua nafasi ya Mbrazil, Marcio Maximo aliyeondolewa baada ya kutofautiana na uongozi.
  Pluijm atafanya kazi na aliyekuwa Msaidizi wake awali akifanya kazi Yanga SC msimu uliopita, Charles Boniface Mkwasa baada ya Maximo kuondolewa pamoja na Msaidizi wake, Mbrazil mwenzake, Leonardo Leiva.
  Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Jerry Muro

  Pluijm amesema kwamba ameiona Yanga SC na akiwa ana muda wa wiki moja kabla ya kucheza na mabingwa watetezi, Azam FC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ana muda wa kutosha kurekebisha timu.
  “Nitatumia wiki hii tukiwa kambini kurekebisha timu na kurudisha mfumo wa kucheza kwa kushambulia na kuburudisha kwa soka nzuri, nataka nirejeshe heshima ya Yanga,”amesema.
  Amesema kwamba pamoja na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji kama Waganda, Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza, Mrundi Didier Kavumbangu na mzalendo Frank Domayo, Yanga bado ni timu nzuri.
  “Mnapokuwa familia kubwa, akiondoka mtu mmoja au wawili, haimaanishi ni mwisho wa familia. Mtamkumbuka aliyeondoka, lakini familia itabaki na kuendelea,”amesema.
  Lakini pia amesema Yanga SC imesajili wachezaji wengine wazuri ambao anaamini watawafanya mashabiki wa timu hiyo wawasahau wachezaji walioondoka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM: NITAREJESHA RAHA NA SOKA YA KUSHAMBULIA, KUBURUDISHA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top