• HABARI MPYA

  Sunday, December 28, 2014

  HAKUNA KUPEPESA YANGA NA AZAM LEO TAIFA, JICHO KODO DAKIKA 90

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo zinatarajiwa kuwaka moto kwa mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baina ya mabingwa, Azam FC na washindi wa pili wa msimu uliopita, Yanga SC.
  Timu hizo ambazo kwa misimu miwili iliyopita zimekuwa zikishindania ubingwa wa Ligi Kuu, kwa mara nyingine msimu huu zinaelekea kwenda sawa.
  Azam FC waliipokonya Yanga SC ubingwa msimu uliopita na timu ya Jangwani msimu huu imepania kurejesha taji lake.
  Kushoto ni mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche na kulia ni mabeki wa Yanga SC, Kevin Yondan na Oscar Joshua katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Septemba 14, mwaka huu timu hizo zilipokutana mara ya mwisho.

  REKODI YA YANGA NA AZM FC LIGI KUU: 

  Machi 19, 2014; 
  Yanga SC 1-1 Azam FC
  Septemba 22, 2013; 
  Azam FC 3-2 Yanga SC
  Februari 23, 2013;  
  Yanga SC 1-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
  Novemba 4, 2012;  
  Azam FC 0-2 Yanga SC
  Machi 10, 2012; 
  Yanga SC 1-3 Azam FC
  Septemba 18, 2011;  
  Azam 1-0 Yanga SC
  Machi 30, 2011;  
  Yanga SC 2-1 Azam FC
  Oktoba 24, 2010; 
  Azam FC 0-0 Yanga SC
  Machi  7, 2010;  
  Yanga SC 2-1 Azam FC   
  Oktoba 17, 2009; 
  Azam FC 1-1 Yanga SC
  Aprili 8, 2009;  
  Yanga SC 2-3 Azam FC
  Oktoba 15, 2008;  
  Azam FC 1-3 Yanga SC
  Septemba 14, 2014
  Yanga SC 3-0 Azam FC (Ngao ya Jamii)
  Hadi sasa, Yanga SC na Azam zinalingana kwa pointi 13, kila mmoja baada ya mechi saba na mshindi wa leo anaweza kupanda kileleni au nafasi ya pili, itategemea na matokeo ya mchezo kati ya vinara wa sasa, Mtibwa Sugar na Stand United.
  Mechi kati ya Mtibwa na Stand United ilivunjika dakika ya sita jana kutokana na mvua na sasa itaendelea leo kuanzia dakika ya sita. Mtibwa inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 15.
  Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Septemba 14 mwaka huu na Yanga SC iliilaza Azam FC 3-0.
  Mabadiliko makubwa yapo kwenye kikosi cha Yanga SC kutoka mchezo wa mwisho timu hizo zilipokutana, lakini kwa Azam FC wameongezeka beki Serge Wawa Pascal kutoka Ivory Coast aliyekuwa anachezea El Merreikh ya Sudan na Kocha Msaidizi, Mganda George ‘Best’ Nsimbe aliyechukua nafasi ya Muingereza, Kali Ongala.
  Yanga SC imebadilika kuanzia benchi la Ufundi, ambako makocha Wabrazil Marcio Maximo na Msaidizi wake, Leonardo Leiva wamewapisha Mholanzi Hans van der Pluijm na Msaidizi wake, mzalendo Charles Boniface Mkwasa.
  Lakini pia, Yanga SC imesajili washambuliaji wapya watatu, mzalendo Danny Mrwanda aliyekuwa anacheza Asia, Mrundi Amisi Tambwe mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita kutoka kwa mahasimu Simba SC na Mliberia Kpah Sean Sherman aliyekuwa anacheza Cyprus.  
  Beki wa Yanga SC, Juma Abdul akipambana na mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche Septemba 14, mwaka huu

  Tayari zote Yanga SC na Azam FC msimu huu zimepoteza mechi mbili kila mmoja na kutoa sare moja, zikishinda mechi nne nne kila timu.
  Yanga SC wamefugiwa ugenini mechi zote, 2-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro na 1-0 na Kagera Sugar Bukoba, wakati Azam FC wamefungwa 1-0 nyumbani Azam Complex, Chamazi na JKT Ruvu na 1-0 na Ndanda FC mjini Mtwara. 
  Azam FC inayofundishwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog ilikwenda kuweka kambi ya siku 10 mjini Kampala, Uganda ambako ilipata pia mechi nne za kujipima nguvu, ikishinda moja na kufungwa tatu.
  Timu hiyo inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, iifungwa 3-2 na SC Villa, 2-0 na URA na 1-0 na KCCA, wakati yenyewe iliifunga Vipers FC 3-0.
  Yanga SC imekuwa kambini Bagamoyo tangu wiki iliyopita baada tu ya kufungwa mabao 2-0 na mahasimu Simba SC katika mchezo wa Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mtibwa Sugar wanaongoza Ligi Kuu, lakini bado mechi kati ya Yanga na Azam ndiyo imebeba taswira ya bingwa wa nchi- hivyo mchezo wa leo unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.

  ZILIPOKUTANA MARA YA MWISHO YANGA NA AZAM: 

  SEPTEMBA 14, 2014, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
  YANGA SC imetwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
  Mshambuliaji wa Kibrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ alifunga mabao mawili katika mchezo huo, wakati Simon Msuva alifunga la tatu, yote kipindi cha pili.
  Dakika 45 za kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa hazijafungana na timu zote zilishambuliana kwa zamu.
  Azam ilitawala mchezo dakika 30 za mwanzoni, lakini Yanga ilichangamka baada ya kocha Marcio Maximo kumpumzisha chipukizi Said ‘Kizota’ Juma na kumuingiza Hassan Dilunga aliyekwenda kufanya kazi nzuri.
  Safu ya ulinzi ya Yanga SC leo ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kufanikiwa kuwadhibiti washambuliaji hatari wa Azam FC, akina Leonel Saint Preux, Didier Kavumbangu na Kipre Herman Tchetche.
  Kipindi cha pili, Azam FC walikianza kwa kasi wakifanya mashambulizi mawili mfululizo- lakini safu ya ulinzi ya Yanga SC ilisimama imara kudhibiti hatari zote.
  Winga Simon Msuva aliyeingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Nizar Khalfan ndiye aliyekwenda kuimaliza Azam FC.
  Msuva aliseti bao moja na kufunga moja- kwanza akitia krosi ambayo ilimbabatiza beki wa Azam na kumkuta Jaja aliyefunga dakika ya 56 na baadaye akafunga mwenyewe bao la tatu.    
  Lakini kabla ya Msuva kufunga la tatu, Jaja alifunga tena baada ya kupokea pasi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa na kumchambua vizuri kipa Mwadini Ali dakika ya 65.
  Msuva alifunga bao la tatu baada ya kupokea pasi ndefu ya Hussein Javu na kukutana na kipa Mwadini Ali aliyetoka langoni ambaye alimlamba chenga na kwenda kuukwamisha mpira nyavuni dakika ya 87.
  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick alimkabidhi Nahodha wa Yanga SC Ngao baada ya mechi hiyo na baada ya hapo, wachezaji, viongozi na makocha wa timu hiyo wakaanza kushangilia.
  Hii ni mara ya pili mfululizo Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya mwaka jana pia kuifunga Azam FC 1-0, bao pekee la Salum Telela.    
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Said ‘Kizota’ Juma/Hassan Dilunga dk37, Haruna Niyonzima/Hussein Javu dk79, Genilson Santana ‘Jaja’/Hamisi Kiiza dk79, Mrisho Ngassa/Omega Seme dk72 na Nizar Khlafan/Simon Msuva dk46.
  Azam FC; Mwadini Ali, Erasto Nyoni/Gardiel Michael dk74, Shomary Kapombe, David Mwantika, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao/Kevin Friday dk62, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Didier Kavumbangu, Kipre Tchetche/Ismaila Diara dk83 na Leonel Saint-Preux/Khamis Mcha dk62.  
  Yanga SC wakifurahia na Ngao yao baada ya kuifunga Azam FC Septemba 14, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAKUNA KUPEPESA YANGA NA AZAM LEO TAIFA, JICHO KODO DAKIKA 90 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top