• HABARI MPYA

  Wednesday, December 31, 2014

  SC VILLA WAIKACHA YANGA SC KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SC Villa ya Uganda imejitoa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na Yanga SC wanajikuta katika kundi ‘nyororo’ zaidi pamoja na timu za Taifa Jang’ombe, Polisi na Shaba zote za Zanzibar.
  SC Villa ilitarajiwa kuja kutia nakshi mashindano haya kutokana na upinzani uliopo baina yao na Yanga SC.
  Mara mbili, 1993 na 1999, Yanga SC iliifunga SC Villa katika Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda na kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, sasa hivi ikijulikana kama Kombe la Kagame.  
  Taifa ndiyo imechukua nafasi ya Jogoo la Kampala na itacheza mechi yake ya kwanza na Yanga SC Januari 2, Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Mshambuliaji wa zamani wa SC Villa, Hassan Mubiru (kushoto) akiruka dhidi ya beki wa zamani wa Yanga SC, Bakari Malima 'Jembe Ulaya' katika Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Januari 16, mwaka 1999 Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda. Yanga SC ilishinda kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 120. Mubiru alitangulia kuifungia Villa dakika ya saba, Edibily Lunyamila akaisawazishia Yanga SC dakika ya 42. Iddi Batambuze pekee alifunga penalti ya Villa, nyingine tatu Manyika Peter akizicheza.

  Mapema Saa 9:00 Alasiri, KMKM itamenyana na Mtende na Saa 11:00, mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda watamenyana na mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, Azam FC, zote mechi za Kundi B.  
  Mabingwa wengine wa zamani wa michuano hiyo, Simba SC na Mtibwa Sugar watamenyana kesho katika mchezo wa kukata utepe wa michuano hiyo 2015 Uwanja wa Amaan, kuanzia saa 2:15, huo ukiwa mchezo wa kundi C.
  Pambano hilo linatarajiwa kuwa la marudiano kufuatia timu hizo kufungana bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
  Mchezo huo utatanguliwa na mwengine wa kundi hilo kati ya maafande wa Mafunzo na JKU utakaoanza saa 9:00 mchana.
  Kwa jumla, timu zinazoshiriki mashindano hayo zimepangwa katika makundi matatu, ambapo kundi A linajumuisha timu za Taifa, Yanga SC, Polisi na Shaba, Kundi B KCCA, Azam FC, KMKM na Mtende Rangers na Kundi C kuna Simba SC, Mtibwa Sugar, JKU na Mafunzo.
  Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya robo fainali, na timu mbili zitapatikana kutokana na washindwa waliofanya vizuri (Best Loosers). Fainali ya ngarambe hizo imepangwa kupigwa Januari 13, 2015.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SC VILLA WAIKACHA YANGA SC KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top