• HABARI MPYA

    Sunday, December 21, 2014

    YANGA SC HAWAKUWA NA NAMNA NYINGINE ZAIDI YA KUACHANA NA MAXIMO

    KUNA uhasama kati ya mshambuliaji Emmanuel Okwi na klabu ya Yanga SC kwa sasa.
    Uhasama huo ulianza baada ya mchezaji huyo kurejea klabu yake ya zamani, Simba SC kufuatia kutemwa Yanga SC.
    Yanga SC iliamua kuvunja Mkataba na Okwi na ikaandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiomba Mkataba huo usitambuliwe.
    Yanga SC walikuwa wana sababu ya kufikia hatua hiyo, ambayo ni nidhamu ya mchezaji- kuchelewa kujiunga na timu baada ya ruhusa ya kwenda kwao kwa mapumziko.
    Lakini shinikizo haswa la Yanga SC kuanza mipango ya kuachana na Okwi, lilitokana na aliyekuwa kocha wao, Mbrazil Marcio Maximo.

    Maximo alishinikiza Okwi aachwe ili asajiliwe Mbrazil mwenzake, Genilson Santana Santos ‘Jaja’. Lakini kwa sababu mapema sana, Jaja alionyesha si mchezaji wa kiwango cha Okwi, uongozi wa Yanga SC ulimuomba Maximo aachane naye na Okwi arudishwe.
    Maximo akatishia kuondoka, iwapo Jaja angeachwa na Yanga SC wakati huo walikuwa wanampenda sana kocha huyo, hivyo wakakubaliana naye.
    Baada ya mechi saba za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Maximo na uongozi wa Yanga SC wakajiridhisha Jaja hana tija katika timu.
    Kilichofuatia, Maximo akamuacha Jaja Brazil walipokwenda naye mapumzikoni, akaja na kiungo Emerson  de Oliviera Roque, ambaye naye hakuwa wa kiwango cha kuridhisha.
    Bahati nzuri, uongozi wa Yanga SC katika kusaka mshambuliaji mbadala wa Jaja, wakampata Mliberia, Kpah Sean Sherman na ikabidi sasa klabu hiyo iingie kwenye mtego wa kuacha mchezaji mmoja wa kigeni.
    Maximo akapendekeza Mganda Hamisi Kiiza, ambaye alikuwa ana rekodi nzuri katika klabu hiyo aachwe, huku uongozi ukitaka aachwe Emerson.
    Kwa mara nyingine, Maximo akawazidi nguvu viongozi wa Yanga SC wakamuacha Kiiza.
    Lakini baada ya mechi ya Nani Mtani Jembe Jumamosi iliyopita Yanga SC ikifungwa 2-0 kirahisi na mahasimu, Simba SC, Maximo pamoja na Msaidizi wake, Leonardo Leiva wa Brazil wakatupiwa virago wote.
    Mholanzi Hans van der Pluijm na mzalendo Charles Boniface Mkwasa wakarejesha kazini mara moja.
    Yanga SC ilicheza ovyo Mtani Jembe, kama timu ambayo haina kocha japokuwa ilikuwa ina wachezaji wazuri uwanjani.
    Yeyote aliyeiona Yanga SC, hata kwa mara ya kwanza ikicheza na Simba wiki iliyopita, alisema; “Timu hii haina kocha”.
    Kila kitu kilikuwa ovyo, upangaji wa timu, mabadiliko na hata mfumo siyo haukuwa na tija, bali pia haukueleweka.
    Kuna mambo mengine huhitaji kwenda shule ili kujua ni ya ovyo- unaweza kuyabaini baada ya kuona tu.
    Haihitaji taaluma ya ukocha ili kujua Yanga SC ya Maximo ilikuwa butu- na kwa kiasi kikubwa kiwango kiliporomoka mno kutoka kikosi cha msimu uliopita chini ya Pluijm na Mkwasa.
    Lakini habari za ndani zinasema, Yanga SC walikuwa tayari kuendelea na Maximo, iwapo angekubali kufanya kazi na Mkwasa, lakini yeye alikataa na akasema yuko tayari kuondoka kuliko kufanya kazi na mzalendo huyo.
    Mkwasa ni mwalimu aliyebobea kitaaluma kuliko Maximo japokuwa si Mbrazil- na hata kwa rekodi yeye ni zaidi na hata kwa utendaji yeye ni zaidi. Na zaidi ni mwalimu mzawa anayewajua wachezaji na soka ya Tanzania vizuri mno.
    Sijui kwa nini Maximo alimkataa. Bado, Yanga SC wanasema Maximo alikuwa hashauriki, na alikuwa mwepesi kukiri makosa baada ya athari.
    Mfano suala la Jaja, inaelezwa baadaye Maximo alikiri hakuwa mchezaji mzuri na yeye aliingizwa mkenge na wakala. Kama hivyo ndivyo, kwa nini hakutaka kuusikiliza ushauri wa viongozi wa Yanga SC mapema kwamba Okwi arudishwe katika usajili na Mbrazil mwenzake huyo aachwe?
    Tayari timu imekwishatumia fedha, imepoteza muda kwa mchezaji ambaye hana faida, tu kwa sababu ya ubishi wa kocha.
    Bado ameleta mtu mwingine, Emerson ambaye mapema uongozi umeshituka hana kiwango cha juu, lakini akamkingia kifua hadi akaachwa mchezaji anayefahamika ni mzuri, Kiiza.
    Yaani kwa haya yote unaona kabisa, Yanga SC hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kuachana na Maximo.          
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC HAWAKUWA NA NAMNA NYINGINE ZAIDI YA KUACHANA NA MAXIMO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top