TIMU za Mbeya City na Tanzania Prisons zote za Mbeya – kwa pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro zote zipo hatarini kushuka Daraja baada ya mechi za mzunguko wa 29 leo.
Wakiwa nyumbani, Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya, Tanzania Prisons wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, huku Mbeya City ikitoa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Dodoma Jiji FC Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Baada ya matokeo hayo, Mtibwa Sugar inashukia nafasi ya 15 ikibaki na pointi zake 27, nyuma ya Tanzania Prisons nafasi ya 14 na Mbeya City nafasi ya 13 baada ya timu hizo zote kucheza mechi 29 zikiwa hatarini kuungana na KMC FC ambayo tayari imeshuka daraja.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, mabingwa watetezi, Yanga SC wamelikaribia taji la tano mfululizo la Ligi Kuu baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Nao Simba SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars Uwanja wa Meja Jenerali Charles Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam huku Azam FC ikiichapa Coastal Union mabao 2-0 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Nayo JKT Tanzania imewachapa wenyeji Pamba Jiji FC mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, Mashujaa FC imeilaza KMC FC 2-0 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma na Namungo FC imetoa sare ya 0-0 na Fountain Gate Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.




.png)
0 comments:
Post a Comment