TIMU ya Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Meja Jenerali Charles Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Prince Mpumelelo Dube dakika ya nane, kiungo Maxi Mpia Nzengeli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurélio ‘Depu’ kutoka Angola dakika ya 66.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inamaliza Ligi Kuu msimu wa 2025 – 2026 ikiwa na pointi 75, mbili Zaidi ya watani wao, Simba SC waliomaliza nafasi ya pili baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, KMC FC jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Hilo linakuwa taji la tano mfululizo la Ligi Kuu kwa Yanga kuanzia msimu wa 2021–2022, 2022–2023, 2023–2024 na 2024–2025 na hiyo inakuwa mara ya pili kwa wana Jangwani hao kutwaa mataji ya Ligi Kuu mara tano mfululizo baada ya kufanya hivyo misimu ya 1968, 1969, 1970, 1971 na 1972.
Kwa ujumla hilo linakuwa taji la 32 la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa Yanga – pamoja nay ale iliyobeba kwenye misimu ya 1974, 1981, 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2012–2013, 2014–2015, 2015–2016 na 2016–2017.
Timu nyingine iliyowahi kutwaa taji la Ligi Ku umara tano mfululizo ni watani wao, Simba SC waliofanya hivyo mara moja kuanzia msimu wa 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980, ambao pia wanafuatia kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu kwa ujumla, 22 mengine miaka ya 1965, 1966, 1973, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2003, 2004, 2007, 2009–2010, 2011–2012, 2017–2018, 2018–2019, 2019–2020 na 2020–2021.
Matokeo ya mechi nyingine za kuhitimisha msimu wa Ligi Kuu leo; bao la kiungo Mkongo, Inno Jospin Loemba kwa penalti dakika ya 55 limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, KMC Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Nayo Azam FC imeshinda 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji FC mabao ya mshambuliaji Jean-Jacques Ngita kutoka DRC dakika ya 67 na beki wa kulia, Nathaniel Raphael Chilambo dakika ya 90 na ushei Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Namungo FC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, mabao yake yakifungwa na vungo Geoffrey Julius Luzendaze dakika ya 33 na Jacob Raymond Masawe dakika ya 85, huku la wageni likifungwa na beki Fabian Evance Mwalugala dakika ya kwanza Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.
Bao la mkwaju wa penalti la beki Héritier Baraka Lulihoshi kutoka DRC dakika ya 90 limeipa Tanzania Prisons ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mashujaa FC Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Coastal Union imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Pamba Jiji Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Fountain Gate FC imeichapa Singida Black Stars mabao 4-3 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, huku Mbeya City ikilazimishwa sare ya bila mabao TRA United Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Jijini Arusha mabao ya Fountain Gate FC yamefungwa na Wanigeria, kiungo Henry David dakika ya tano, mshambuliaji Obasi MacDonald Chukwunonye dakika ya 26 na mshambuliaji chipukizi, Hashimu Omary Kindemile aliyefunga mawili dakika ya 66 na 67, huku ya Singida Black Stars yote yakifungwa na winga Mossi Nduwumwe matatu dakika ya tisa, 12 na 86.
Matokeo hayo yanamaanisha Yanga inamaliza kileleni kwa pointi zake 75, ikifuatiwa na Simba 73 na zote zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, Azam FC pointi 64 na Singida Black Stars 50 na zote zitacheza Kombe la Shirikisho Afrika.
TRA United wenye pointi 43 wamemaliza nafasi ya tano waifuatiwa na JKT Tanzania wenye pointi 42, Pamba Jiji FC pointi 36 sawa na Coastal Union, Dodoma Jiji pointi 35, Namungo FC pointi 34, Mashujaa FC pointi 33 sawa na Fountain Gate FC nazo zinasalia Ligi Kuu msimu ujao.
Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi zao 32 itamenyana na ndugu zao, Mbeya City waliomaliza na pointi 30 katika mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu msimu ujao.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu iliyofuzu kwenye mchujo wa Ligi ya Championship kwa mechi mbili pia za nyumbani na ugenini kuwania kucheza Ligi Kuu msimu ujao – na itakayofungwa itacheza Championship, wakati Mtibwa Sugar iliyomaliza na pointi 27 inaungana na KMC FC kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu.



.png)
0 comments:
Post a Comment