• HABARI MPYA

  Wednesday, December 31, 2014

  VIONGOZI SIMBA SC SASA WAJITATHMINI NA WAO WENYEWE

  KATIKA kipindi cha nusu mwaka tangu uongozi wa Simba SC kuwa madarakani chini ya Rais, Evans Elieza Aveva kocha wa tatu anatarajiwa kuanza kazi mapema iwezekanavyo.
  Mserbia Goran Kopunovic anawasili asubuhi ya leo Dar es Salaam kwa ajili ya kusaini Mkataba wa kuifundisha klabu ya Simba, kurithi mikoba ya Mzambia, Patrick Phiri anayeondolewa.
  Na Kopunovic anatarajiwa kusaidiwa na Mnyarwanda, Jean Marie Ntagawabila- maana yake Suleiman Matola naye aliyekuwa msaidizi wa Phiri ataondolewa pia.
  Kopunovic alifanya kazi kwa mafanikio nchini Rwanda akiwa na klabu ya Polisi kwa miaka mitatu kabla ya kuhamia Vietnam ambako pia alifanya kazi kwa mafanikio na hakuna shaka huyo ni kocha bora.

  Kocha huyo anayefundisha soka maridadi ya kuburudisha, kushambulia sifa yake kubwa ni wachezaji wake kuwa na nguvu na kasi kutokana na aina ya mazoezi anayowapa.
  Kwa Ntagawabila, huyo ni kocha mwenye heshima kubwa Rwanda ambaye wakati fulani aliifanya APR iwe tishio mno kiasi cha kufikia kuifunga Zamalek ya Misri mabao 4-1 mwaka 2004 katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikitoka kufungwa 3-2 katika mchezo wa kwanza Cairo.
  APR ilisonga mbele hatua ya 16 Bora, ambako ilikwenda kutolewa kwa mbinde na Africa Sports ya Ivory Coast kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Simba SC inafikia hatua ya kuachana na Phiri baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu chini yake tangu ameanza kazi Agosti mwaka huu akirithi mikoba ya Zdravko Logarusic raia wa Croatia.
  Simba SC iliachana na Logarusic kwa sababu tu ya tabia zake za kifedhuli, ambazo ilijaribu sana kumkemea, lakini hakuwa tayari kubadilika na ikaamua kumrejesha Phiri kutokana na historia yake ya kufanya kazi kwa mafanikio awali katika klabu hiyo. 
  Hata hivyo, safari hii mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa baina ya Phiri na Simba SC na ndoa yao inafikia tamati, Kopunovic akiingia kazini.
  Phiri aliiongoza Simba SC kwa mara ya mwisho Desemba 26, ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Tangu amekuja Simba SC kwa mara ya tatu Agosti mwaka huu, Phiri ameiongoza Simba SC katika mechi 22 na kushinda nane, kati ya hizo moja tu ya Ligi Kuu 1-0 dhidi ya Ruvu Shooitng na moja ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga SC 2-0, wakati amefungwa tano na kutoka sare tisa.
  Kweli, Logarusic alikuwa ana kashfa ya kukosa uadilifu tangu akiwa anafundisha Gor Mahia ya Kenya, tabia ambayo alikuja kuiendeleza Dar es Salaam na uongozi mpya wa Simba ukashindwa kuivumilia.
  Ikumbukwe Logarusic aliajiriwa na uongozi uliopita chini ya Rais, Alhaj Ismail Aden Rage na akabahatika kupewa Mkataba mpya chini ya uongozi mpya wa Aveva.
  Hata hivyo, wiki mbili baadaye Loga akafukuzwa timu ikitoka kufungwa mabao 3-0 na Zesco United ya Zambia katika mchezo wa kirafiki.
  Rahisi kumshawishi mtu ulikuwa sahihi kumfuta kazi kocha asiye mwadilifu- hususan kama kuna ushahidi hadi Kenya.
  Na kwa Phiri pia, baada ya kushinda mechi moja tu kati ya nane za Ligi Kuu, kweli hii haikuwa rekodi nzuri na si ajabu kwa kocha wa aina hiyo kuondolewa kazini.
  Ndiyo maana tangu kuvuja kwa habari za Phiri kuondolewa kazini, wengi miongoni mwa wapenzi wa Simba SC wameridhishwa na uamuzi huo.
  Wanaona timu yao imesajili wachezaji wazuri, inapatiwa maandalizi mazuri, lakini kwenye Ligi Kuu haipati matokeo mazuri- hivyo hawana hamu na mwalimu.
  Lakini wana Simba SC wanafahamu katika kipindi cha nusu mwaka chini ya uongozi wa Aveva, timu itakuwa chini ya kocha wa tatu.
  Hii ni idadi kubwa mno kwa kipindi kifupi namna hiyo- lakini tu sababu kama za Loga kuondolewa na Phiri zinaweza kuwashawishi watu kukubaliana na kilichotokea, si tatizo sana.
  Ila sasa, viongozi wa Simba SC wakae wakijua kwamba, ujio wa kocha mpya, na wa tatu katika kipindi kifupi cha nusu mwaka ni changamoto nyingine kwao, tena kubwa sana.
  Haitakuwa rahisi watu kukubali tena kwamba tatizo la matokeo mabaya litakuwa kocha chini ya mwalimu wa tatu kutoka Serbia.
  Huu ni wakati sasa uongozi wa Simba SC kujiangalia mara mbili, kujitathmini juu ya mwenendo wao wa kiuongozi na uwajibikaji kwa ujumla, kama kuna sehemu wana mapungufu, wajirekebishe. Heri ya mwaka mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VIONGOZI SIMBA SC SASA WAJITATHMINI NA WAO WENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top