• HABARI MPYA

  Thursday, December 11, 2014

  HATIMA YA SHERMAN KUJULIKANA LEO YANGA SC

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Liberia, Kpah Sean Sherman leo anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya, ambavyo akifuzu atasaini Mkataba wa kujiunga na klabu ya Yanga SC.
  Mliberia huyo aliyewasili jana Dar es Salaam na kufikia katika hoteli moja ya nyota tatu, atakutana na uongozi wa Yanga SC Saa 4:00 asubuhi ya leo kwa ajili ya kwenda hospitali kwa zoezi hilo.
  Kwa pamoja, Yanga SC na mchezaji huyo wana matumaini makubwa mambo yatakwenda vizuri na watafunga ndoa ya mwaka mmoja.
  Kpah Sherman atafanyiwa vipimo vya afya leo asubuhi
  Na iwapo mambo yatakwenda vizuri na zoezi la Mkataba likamalizika mapema, Sherman anaweza kuanza mazoezi jioni ya leo Yanga SC na kuingia kambini moja kwa moja.
  Mwenyewe alipowasili jana, Sherman alisema; “Nina furaha sana kufika hapa salama, natarajia kila kitu kitakwenda vizuri na nitakuwa mchezaji wa Yanga. Nipo tayari kukabiliana na changamoto mpya,”amesema. 
  Sherman mwenye umri wa miaka 22 ametua Yanga SC akitokea klabu ya Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini, ambako analazimika kuvunja Mkataba wake uliobakiza miezi minne.
  Alianza kuichezea Cetinkaya mwaka 2012, akitokea Duzkaya SK aliyoanza kuichezea mwaka 
  2010, akitokea Barrack YC ya nyumbani kwao, Liberia ambayo alianza kuichezea mwaka 2009.
  Sherman akifanikiwa kusaini Yanga SC, atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa dirisha la dogo baada ya kiungo mkabaji Mbrazil, Emerson de Oliviera Roque na mshambuliaji mzalendo, Danny Mrwanda aliyekuwa anacheza Vietnam.
  Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Yanga SC kama itamsajili Sherman mkali wa mabao katika Ligi ya Cyprus Kaskazini, italazimika kukata mchezaji mmoja wa kigeni ili ikidhi kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotaka wageni watano tu.
  Bila ya Sherman, tayari Yanga SC inao Wabrazil Emerson, Andrey Coutinho, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite na Mganda Hamisi Kiiza.  
  Aidha, Sherman akisajiliwa Yanga SC atakuwa Mliberia wa pili kucheza Tanzania, baada ya William Fahnbullar aliyewika Simba SC kuanzia 1997 hadi 1999 alipohamia Kajumulo WS kabla ya kutimkia Ulaya.
  Yanga SC kwa sasa ipo kambini katika hoteli ya Landmark, eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam ikijiandaa na mechi ya Nani Mtani Jembe 2 Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HATIMA YA SHERMAN KUJULIKANA LEO YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top