• HABARI MPYA

  Wednesday, December 10, 2014

  HAPA NDIPO ULIPOLALIA MSINGI WA MATATIZO YA SOKA YETU

  KATIKA siku ya kusherehekea miaka 53 ya Uhuru wa taifa letu, jana uliandaliwa mchezo wa kirafiki baina ya kikosi cha pili cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, maarufu kama ‘Taifa Stars Maboresho’ dhidi ya Burundi.
  Maboresho inayoundwa na vijana wengi wadogo waliobuka na kuibuliwa miaka ya karibuni, ilifungwa mabao 2-1 na Burundi katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mechi hiyo maalum iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusherehekea miaka 53 ya Uhuru, Stars Maboresho ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 11 kupitia kwa Yussuf Rashid.

  Burundi walichangamka baada ya bao hilo na kuanza kusukuma mashambulizi ya nguvu langoni mwa Maboresho iliyoongozwa na Kocha Mkuu wa Tanzania, Mholanzi Mart Nooij.
  Kwa kutumia vyema udhaifu wa safu ya kiungo ya Tanzania, Burundi walitawala mchezo na kufanikiwa na kupata bao la kusawazisha dakika ya 25, mfungaji Fabrice Mimimahazwe kabla ya kupata bao la ushindi dakika ya 72 kupitia kwa Nassor Niyonkuru.
  Maboresho walicharuka baada ya kufungwa bao la pili na kuanza kushambulia mfululizo, lakini kipa wa Burundi, Innocent Mbonihankuye alikuwa kikwazo kwao kupata bao.
  Kwa ujumla, Stars Maboresho haikucheza soka ya kuvutia na maana yake Mart Nooij ana kazi kubwa ya kufanya kuiboresha timu hiyo.  
  Vijana wetu wadogo waliobuliwa maka ya karibuni kama Kikosi cha Tanzania kilikuwa Miraj Adam, Gardiel Michael, Joram Mgeveke, Salum Mbonde, Hassan Banda, Atupele Green, Kelvin Friday na wengine walishindwa kucheza vizuri kama ilivyotarajiwa.
  Tatizo nini? Mashabiki mmoja mmoja na baadhi ya Vyombo vya Habari vilipeleka lawama kwa baadhi ya wachezaji kwamba hawakucheza vizuri. Hawakukosea, walikuwa sahihi, lakini tumekwishajua tatizo letu ni nini maana soka yetu imekuwa ugonjwa wa moyo kwa miaka kadhaa sasa.
  Kwa sasa, ukiitisha mashindano ya vijana Tanzania wakati wowote, iwe chini ya umri wa miaka 15, miaka 17 hata 20, zitajitokeza timu za kutosha na zilizo tayari kushiriki.
  Mpira unachezwa kwa kiasi kikubwa kwa sasa Tanzania, kuanzia mijini na vijijini na haya ni matunda ya mashindano ya vijana yaliyo katika mfumo wa kitaifa kama Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars.
  Inakuwa rahisi mno kwa klabu za Ligi Kuu kupata wachezaji wa kuunda timu zao za vijana. Inakuwa rahisi mno katika uundwaji wa timu za taifa za vijana- kwa sababu tayari vipaji vimekwishaibuliwa.
  Leo huhitaji kufoji mchezaji kijeba katika mashindano ya vijana- kwa sababu wachezaji wenyewe vijana halisi wapo.
  Tumetoka mbali, wakati ambao taifa zima lilitegemea shule ya Makongo pekee kama kituo cha kulea vipaji vya vijana.
  Leo hii shule kadhaa nchini zinasaidia mpango wa soka ya vijana, kuna vituo vingi vijana wanacheza. Kuna timu nyingi za vijana nchini, tena za ushindani.
  Baadhi ya klabu zina programu nzuri za soka ya vijana mfano Azam FC na timu za majeshi, hususan za Jeshi la Kujenga la Taifa (JKT).
  Lakini bado tunakabiliwa na tatizo moja kubwa la msingi- tunaibua vipaji kwa wingi, baada ya hapo inakosekana fursa ya kuwaendeleza vijana.
  Hakuna mashindano maalum ya vijana kucheza kwa muda mrefu, ili kuwajengea uwezo wa kushindana na kuwakomaza kwa ujumla.
  Kanuni za Ligi Kuu zinaelekeza kila klabu inapaswa kuwa na timu ya vijana, tena wachezaji wanasajiliwa rasmi kwa ajili ya kucheza ligi yao.
  Lakini ligi hiyo ya vijana imeshindwa kufanikiwa kwa sababu, timu hazisafiiri kama ilivyo kwa timu za wakubwa, zinacheza mechi nyumbani tu.
  Kwa sababu Dar es Salaam kuna Simba, Yanga, Azam, JKT Ruvu, basi na timu za vijana na klabu hizo zitakutana kabla ya wakubwa zao kucheza mechi za Ligi Kuu.
  Kikubwa kinachoelezwa na klabu ni kwamba, hawana uwezo wa kusafirisha timu za vijana kwa sababu ligi hiyo ya vijana haina mdhamini.
  Matokeo yake sasa, klabu za Ligi Kuu timu zao zote za vijana hukutanishwa katika mashindano ya wiki mbili ya mtoano kutafuta bingwa, maarufu kama Kombe la Uhai, ambayo nayo mwaka huu hayakufanyika.
  Baadhi ya timu zitaweza kushiriki mashindano mengine kama Kombe la Rollingston ambayo pia ni michuano ya mtoano ya wiki mbili.
  Mchezaji akijirudia kwenye Kombe la Uhai mara tatu, tayari ataitwa mzee, kwa sababu amecheza mashindano hayo kwa miaka mitatu. Lakini hatujiulizi katika kipindi hicho amecheza mechi ngapi?
  Tumekuwa tukiona timu zetu za vijana za taifa, hazifanyi vizuri katika michuano ya kufuzu kwa Fainali za Afrika tu kwa sababu wachezaji wake wanazidiwa uwezo na wenzao.
  Wanazidiwa uwezo na wenzao ambao wanaonekana wamekomaa zaidi kisoka, japokuwa kiumri hakuna tofauti- sababu wenzao wanacheza sana mashindano, kitu ambacho wao wanakosa.
  Julai 17, mwaka huu tuliona U17 yetu ikitolewa jasho na U17 ya Afrika Kusini pale Chamazi- wachezaji walionekana kabisa kulingana umri, lakini Amajimbos walituzidi kimchezo.
  Vijana wetu walionyesha wana vipaji pia, lakini walionekana kuzidiwa uwezo na wenzao- tu kwa sababu Amajimbos wanacheza sana mashindano na vijana wetu hawaipati fursa hiyo.
  Angalia jana kwa mfano, mchezaji kama Kefin Friday, ndiyo alikwishapandishwa timu ya wakubwa ya Azam FC, lakini muda mrefu sasa hana namba kikosi cha kwanza tena.
  Hachezi Azam Academy, hachezi Azam ya wakubwa, kuna ajabu gani kiwango chake kuonekana kimeshuka jana? Kadhali na wengine kama Miraj Adam, pia amepoteza namba kikosi cha kwanza cha Simba SC kwa muda sasa, maana yake ndiyo sababu ya kushuka kwake.
  Ukweli ni kwamba tumepiga hatua katika dhana ya uwekezaji kwenye soka ya vijana kutoka enzi zile za kuchomekea vijeba- hadi sasa watoto halisi wamesheheni tayari kwa mashindano.
  Lakini tunahitaji sasa kufikiria namna ya kumuendeleza kijana baada ya kumuibua kwa kuhakikisha anacheza mashindano.
  Kwanza, ni kuwa programu maalum kwa vijana waliobuliwa na kuwekwa katika kundi la kuendelezwa ili kesho waje kuwa wachezaji tegemeo wa nchi.
  Lazima maendeleo yao yafuataliwe katika klabu zao na kama kuna tatizo lipatiwe ufumbuzi. Kama mcheaji hana nafasi katika yake, atolewe kwa mkopo sehemu nyingine ambako atakwenda kucheza. 
  Lakini pia, namna nyingine nzuri ambayo TFF wanapaswa kufanya kwa sasa chini ya rais wake, Jamal Malinzi ni kuhakikisha kunakuwa na ligi madhubuti ya vijana, vinginevyo timu zetu za taifa za vijana zitaendelea kuwa dhaifu mbele ya vijana wenzao walioiva. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAPA NDIPO ULIPOLALIA MSINGI WA MATATIZO YA SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top