• HABARI MPYA

  Friday, December 12, 2014

  SHERMAN AANGUKA MIAKA MIWILI YANGA SC

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Liberia, Kpah Sean Sherman amesaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na Yanga SC jioni ya leo mjini Dar es Salaam.
  Kwa kusaini Mkataba huo, Sherman anakuwa Mliberia wa pili kucheza Tanzania, baada ya William Fahnbullar aliyewika Simba SC kuanzia 1997 hadi 1999 alipohamia Kajumulo WS kabla ya kutimkia Ulaya.
  Mshambuliaji huyo mwenye mrefu mwenye umbo kubwa, ambaye jana alikabidhiwa jezi namba 25 aliyokuwa anavaa Mganda Emmanuel Anold Okwi wakati yupo Yanga SC, sasa anatarajiwa kuichezea timu hiyo dhidi ya Simba SC kesho.  
  Okwi alirejea Simba SC Agosti, baada ya kuichezea Yanga SC tangu Desemba- na japokuwa alikuwa hajamaliza Mkataba, lakini mgogoro baina yake na klabu hiyo ulimfungulia milango ya kutoka.
  Yanga SC imefuata taratibu zote za kisasa katika kumsajili mchezaji huyo, ikianza na vipimo vya afya leo, utimamu wa mwili na baadaye kwenda kujaribiwa kidogo Uwanja wa Boko Veterani.
  Kpah Sean Sherman kushoto akisaini Mkataba wa Yanga SC. Kulia ni Wakili wa Yanga SC, Frank Macha na katikati ni wakala wa mchezaji huyo, Gibby.


  Yanga SC itamenyana na Simba SC kesho katika mchezo wa Nani Mtani Jembe Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Sherman mwenye umri wa miaka 22 amejiunga na Yanga SC akitokea klabu ya Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini, ambako analazimika kuvunja Mkataba wake uliobakiza miezi minne.
  Alianza kuichezea Cetinkaya mwaka 2012, akitokea Duzkaya SK aliyoanza kuichezea mwaka 
  2010, akitokea Barrack YC ya nyumbani kwao, Liberia ambayo alianza kuichezea mwaka 2009.
  Sherman anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa dirisha la dogo Yanga SC baada ya kiungo mkabaji Mbrazil, Emerson de Oliviera Roque na mshambuliaji mzalendo, Danny Davis Mrwanda aliyekuwa anacheza Vietnam.
  Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu Yanga SC baada ya kumsajili Sherman mkali wa mabao katika Ligi ya Cyprus Kaskazini, italazimika kukata mchezaji mmoja wa kigeni ili ikidhi kanuni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inayotaka wageni watano tu.
  Pamoja na Sherman, wageni wengine Yanga SC ni Wabrazil Emerson, Andrey Coutinho, Wanyarwanda Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite na Mganda Hamisi Kiiza.  
  Tayari mshambuliaji Mganda, Kiiza ameondoka kambini, hoteli ya Landmark, Mbezi Beach, Dar es Salaam leo, akiamini yeye ndiye anayeondolewa katika usajili, ingawa uongozi haujatoa tamko lolote hadi sasa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SHERMAN AANGUKA MIAKA MIWILI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top