• HABARI MPYA

  Tuesday, December 02, 2014

  SSERUNKUMA ATUA DAR NA KUSAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Daniel Muzeyi ‘Dan’ Sserunkuma ametua Dar es Salaam leo na kusaini Mkataba wa miaka miwili kuichezea klabu bingwa ya zamani Tanzania, Simba SC.
  Awali, Sserunkuma alikuja Dar es Salaam wiki iliyopita na kufanya mazungumzo kisha kuahidi kurejea kesho, lakini leo rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva amesema; “Imebidi aje haraka kusaini, kwa sababu ambazo zlikuwa nje ya uwezo wetu, na wake pia,”.
  Aveva amesema mzaliwa huyo wa Desemba 4, mwaka 1989 mjini Kampala, Uganda amesaini Mkataba huo baada ya kumaliza Mkataba na klabu ya Gor Mahia ya Kenya.
  Rais wa Simba SC, Aveva kushoto akiwa na Sserunkuma kulia wakati wa kusaini Mkataba huo leo Dar es Salaam

  Sserunkuma ni mchezaji aliyezaliwa na kukulia wilaya ya Lubega mjini Kampala na alisoma shule maarufu iliyoibua vipaji vya nyota wengi Uganda, St. Mary's ya Kitende.
  Nyota kibao wanaotamba kisoka Uganda wamepita shule hiyo kama Joseph Owino, David Obua, Eric Obua, Emmanuel Okwi na Ibrahim Juma.
  Pia utotoni mwake, alipitia katika akademi ya Friends of Football akiwa ana umri wa miaka 10, kabla ya kuchezea Express kuanzia 2008 hadi 2011 alipohamia Victors alikocheza hadi 2012 alipokwenda Kenya kujiunga na Nairobi City Stars hadi mwaka 2012 alipotua Gor Mahia.
  Sserunkuma ni mfungaji bora mara mbili mfululizo kwa misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu ya Kenya, wakati pia mwaka 2012 alikuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya nchi hiyo.
  Mwaka 2013, Sserunkuma alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (USPA) Uganda, akiwapiku Tony Mawejje aliyekuwa anacheza Norway na mshambuliaji wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbarara (MUST), Siraje Muhindo.
  Aveva akizungumza na BIN ZUBEIRY wakati Sserunkuma anasaini

  Sserunkuma anachukua nafasi ya majeruhi Mkenya, Paul Kiongera ambaye Simba SC imeamua kumuondoa katika usajili hadi hapo atakapopona goti kuanzia Machi mwakani, ili arejeshwe kwa ajili ya msimu ujao.
  Wachezaji wengine wa kigeni Simba SC ni Waganda Joseph Owino, Emmanuel Okwi na Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe- ambao pamoja na Sserunkuma wanakamilisha idadi ya kikanuni ya Ligi Kuu ya wachezaji watano wa nje.
  Lakini tayari kiungo mshambuliaji wa Gambia, Omar Mboob yuko kwenye majaribio Simba SC tangu jana na kama akifuzu anaweza kuchukua nafasi ya Kiongera, ambaye hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SSERUNKUMA ATUA DAR NA KUSAINI MIAKA MIWILI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top