• HABARI MPYA

    Wednesday, June 24, 2026

    NGOY APIGA HAT-TRICK NAMUNGU YAICHAPA KMC 3-2 PALE PALE MWENGE


    TIMU ya Namungo FC imeibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya wenyeji, KMC FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam. 
    Pongezi kwa mshambuliaji Fabrice Ngoy wa Ngoy kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyefunga mabao yote matatu ya Namungo FC dakika za 18, 24 na 52, huku mabao ya KMC FC yakifungwa na winga Edson Erick Mwijage dakika ya 36 na Mohamed Abdallah dakika ya 70.
    Mechi nyingine za Lig Kuu mabingwa watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam FC Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar jioni ya leo.
    Mabao ya Yanga yamefunwa na beki Ibrahim Hamad Abdullah ‘Bacca’ dakika ya 41, mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurélio  ‘Depu’ kutoka Angola dakika ya 73 na kiungo Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 81.
    Nayo Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
    Mabao ya Simba SC yamefungwa na beki Rushine De Reuck kutoka Afrika Kusini kwa penalti dakika ya tisa, mshambuliaji mzawa, Suleiman Abdallah Mwalimu dakika ya 77 na winga Muivory Coast, Alain Anicet Oura dakika ya 90
    Nayo Singida Black Stars imeichapa Tanzania Prisons mabao 3-1 Uwanja wa Airtel Mwigulu mjini Singida. Mabao ya Singida Black Stars yamefungwa na winga Mrundi Mossi Nduwumwe dakika ya pili na 61 na beki Kennedy Wilson Juma dakika ya 23 huku la Prisons likifungwa na mshambuliaji Kelvin Sengati dakika ya 49.
    Nayo TRA United imetoa sare ya kufungana bao 1-1 na Coastal Union Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha mabao yote yakipatikana kwa mikwaju ya penalti. Beki Nasri Kombo alianza kuifungia TRA United dakika ya 54 kabla ya mshambuliaji Maabad Maulid kuisawazishia Coastal Union dakika ya 68.
    Mshambuliaji Eliud David Ambokile alifunga mabao yote dakika ya 18 na 76, Mbeya City ikiibuka na ushindi wa ugenini wa 2-0 dhidi ya Pamba Jiji FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Naye mshambuliaji Hussein Juma Mihambo akaifungia bao pekee Mashujaa FC dakika ya 86 ikiwalaza wenyeji, Fountain Gate 1-0 Uwanja wa Black Rhino Academy, Karatu, huku Dodoma Jiji FC ikitoa sare ya 0-0 na JKT Tanzania Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.


    Next
    This is the most recent post.
    Older Post
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGOY APIGA HAT-TRICK NAMUNGU YAICHAPA KMC 3-2 PALE PALE MWENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top