• HABARI MPYA

  Jumatano, Januari 06, 2021

  SIMBA SC WAITANDIKA FC PLATINUMS 4-0 NA KUTINGA HATUA YA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA

  Na Shishira Mnzava, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa Tanzania, Simba SC wamefanikiwa kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya FC Platinums ya Zimbabwe leo Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
  Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 4-1 kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumatano iliyopita mjini Harare na kwa kuingia hatua ya makundi itapata Dola za Kimarekani 550,000, zaidi ya Sh Bilioni 1.2.
  Hii inakuwa mara ya tatu kwa Wekundu hao wa Msimbazi kutinga hatua ya makundi baada ya mwaka 2003 walipoitoa Zamalek ya Misri waliokuwa mabingwa watetezi na 2018 walipoitoa Nkana FC ya Zambia.

  Simba SC inayofundishwa na Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Erasto Edward Nyoni kwa penalti dakika ya 39 baada ya beki mwenzake, Shomari Salum Kapombe kuvutwa jezi na Tawana Chikore.
  Kipindi cha pili Kapombe akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 61 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Francis Tizayi kufuatia shuti la kiungo Mzambia Rally Bwalya.
  Nahodha John Raphael Bocco aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwenzake, Mnyarwanda Meddie Kagere akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 90 na ushei akimalizia pasi ya Bwalya tena.
  Mzambia mwingine, Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Tanzania, kiungo Clatous Chotta Chama akaifungia Simba SC bao la nne kwa penalti dakika ya 90 na ushei baada yay eye mwenyewe kuvutwa kwenye boksi na Gift Bello 
  Kagere aliingia dakika ya 76 kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwingine, Mkongo Chris Mutshimba Kope Mugalu lakini akaumia dakika ya 85 na nafasi yake ikachukuliwa Bocco.
  Baada ya msimu mbaya uliopita timu za Tanzania, Simba na Azam FC zikitolewa mapema michuano ya Afrika – hatimaye mwaka huu mambo mazuri, kwani na Namungo FC imetinga kwneye mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. 
  Namungo FC imefanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya sare ya 3-3 na wenyeji, na Al Hilal Obayed jana Uwanja wa Al-Hilal mjini Omdurman, Sudan.
  Kwa matokeo hayo Namungo FC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-3 na sasa itamenyana na moja ya timu zitakazotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Droo ya hatua ya makundi ya michuano hiyo itafanyika Ijumaa Saa 8:00 mchana makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Cairo, Misri.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Rally Bwalya, Said Ndemla/Ibrahim Ame dk60, Chris Mugalu/Meddie Kagere dk76/John Bocco dk85, Clatous Chama na Luis Miquissone.
  FC Platinums; Francis Tizayi, Gift Mbweti, Nomore Chinyerere, Gift Bello, Ralph Kawondera, Donald Dzvinyai, Kelvin Madzongwe, Rahman Kutsanzira, Khumalo Denzel/Raphael Muduviwa dk58, Perfect Chikwende na Tawana Chikore. 

  ZAWADI ZA LIGI YA MABINGWA
  NAFASIZAWADI
  BingwaDola za Kimarekani  Milioni 2.5 
  Mshindi wa piliDola za Kimarekani Milioni 1.25 
  Nusu FainaliDola za Kimarekani 875,000
  Robo FainaliDola za Kimarekani 650,000
  Nafasi ya tatu kundiniDola za Kimarekani 550,000
  Nafasi ya nne kundiniDola za Kimarekani 550,000
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAITANDIKA FC PLATINUMS 4-0 NA KUTINGA HATUA YA MAKUNDI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top