• HABARI MPYA

    Tuesday, January 19, 2021

    NAIBU WAZIRI WA MICHEZO, ULEGA AZITAKA TAASISI ZA MICHEZO KUVUTIA UWEKEZAJI

    Na Grace Semfuko, MAELEZO 
    NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Abdallah Ulega amezitaka  Taasisi zinazosimamia michezo nchini kujituma katika kuimarisha michezo ili kuvutia uwekezaji Zaidi kwenye sekta hiyo.
    Pia amezitaka taasisi hizo kuwajibika na kuwa wawazi katika shughuli zao hatua ambayo itazifanya taasisi mbalimbali zilizowekeza nchini kuchangia michezo hususan katika kuibua vipaji vya vijana.
    Aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam jana katika hafla ya kutoa ufadhili wa masomo ya ufundi kwa vijana 26 wenye umri wa kuanzia miaka 16-19 waliofanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Taifa la Mpira wa Kikapu la Benki ya CRDB, michuano iliyofanyika Novemba 12 na 13 kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma na kushirikisha timu 36 za Wavulana na Wasichana.


    “Nayataka Mashirikisho yetu yote ya michezo mbalimbali Tanzania, na Baraza letu la Michezo, muwe wawazi kuonesha kwamba ninyi mmedhamiria kweli kuendesha shughuli za michezo kwa mafanikio, watu wanapoleta pesa zao kwa shuguhuli za michezo waone zinaleta matunda, janja janja ya aina yoyote ile zinawarudisha nyuma, mfadhili anapoleta fedha anataka kujua zinatumikaje, sasa zinapoliwa watu wanakuwa wagumu sana kuleta fedha zao kwa sababu ya watu wanaosimamia shughuli za michezo kutokuwa waaminifu” amesema Ulega.
    “Sisi Serikali tunawataka muwe wawazi ili kuvutia uwekezaji kwenye michezo, Pesa zipo nyingi kwenye sekta binafsi, na wapenzi wa michezo wapo wengi katika sekta hiyo, wanatafuta sehemu ya kupeleka pesa zao kwenye michezo, lakini kila wakichungulia hivi wakiona usalama wa pesa zao haupo wanahofu kwamba huu mzigo ukifika tu, watu watafanya shoping kidogo, hii ni changamoto kubwa”
    Aidha Ulega aliziomba taasisi zilizowekeza nchini kufadhili sekta ya michezo kama kipaumbele hasa katika suala zima la uwajibikaji kwa jamii (CSR) ili kuwaandaa vijana na ambao wataliwakilisha vyema Taifa letu katika michuano mbalimbali.
    “Bila ya kuwekeza kwa vijana, tunapoteza muda wetu, tuwatazame hawa kwa karibu sana tusije kupoteza vipaji, sio leo Kaka yangu Magesa hapa akiambiwa kunahitajika vijana wa michezo anaingia mtaani kusaka vijana, lazima tuwe na kanzi data ya vijana waliofundishika kimichezo ili kukuza vipaji.”
    Nae Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB ambao ndio wadhamini wakuu wa Michuzo ya "CRDB Taifa Cup 2020" Bi. Tully Ester Mwambapa amesema wameamua kudhamini michuano hiyo ili kukuza vipaji vya Vijana katika Mpira wa Kikapu.
    Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), Bw. Phares Magesa  amesema kufuatia ufadhili huo wa Benki ya CRDB wameweza kuibua vipaji vingi Zaidi na kuiomba Benki hiyo kuandaa michano hiyo kila mwaka.
    Mashindano ya Taifa ya Mpira wa Kikapu ya Benki ya CRDB yamegharimu Zaidi ya shilingi Milioni 250 huku kati ya hizo, Milioni 50 zimetumika kufadhili masomo ya Ufundi kwa Vijana 26 ambao walifanya vizuri katika michuano hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NAIBU WAZIRI WA MICHEZO, ULEGA AZITAKA TAASISI ZA MICHEZO KUVUTIA UWEKEZAJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top