• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 19, 2021

  TANZANIA YAANZA VIBAYA MICHUANO YA CHAN CAMEROON, YACHAPWA MABAO 2-0 NA ZAMBIA

  Na Mwandishi Wetu, LIMBE
  TANZANIA imeanza vibaya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya kuzabwa mabao 2-0 na Zambia katika mchezo wa Kundi D Uwanja wa Omnisport Jijini Limbe.
  Huo unakuwa mchezo wa sita mfululizo kwa Taifa Stars kucheza bila kushinda tangu ishinde dhidi ya Equatorial Guinea Novemba 15, mwaka 2019 kwenye mechi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. 
  Mechi zilizofuata Stars ilichapwa 2-1 na Libya nchini Tunisia Kufuzu AFCON, ilichapwa 1-0 na Burundi Kirafiki  Dar es Salaam, ikachapwa 1-0 na Tunisia Kufuzu AFCON Tunis, ikatoa sare za 1-1 mfululizo nyumbani na Tunisia Kufuzu AFCON na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kirafiki Uwanja wa Mkapa.
  Kwa matokeo hayo, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije imejiweka njia panda kwenda hatua ya mtoano kwenye mbio za kuwania Kombe la michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.  
  Kwa Zambia inayofundishwa na kocha Mserbia, Milutin Sredojevic imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya ushindi huo wa mabao ya kipindi cha pili.


  Mshambuliaji wa NAPSA Stars, Collins Sikombe alipewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kufunga bao moja na kusababisha la pili.
  Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, alifunga kwa penalti dakika ya 64 baada ya beki mkongwe wa Tanzania, Shomari Kapombe kuunawa mpira kwenye boksi katika harakati za kuokoa, kabla ya kumsetia mshambuliaji wa Nkwazi FC, Emmanuel Chabula kufunga la pili dakika ya 81.
  Taifa Stars itarudi Uwanja wa Omnisport Jijini Limbe Jumamosi kumenyana na Namibia kabla ya na kukamilisha mechi zake za Kundi D kwa kucheza na Guinea Uwanja wa Reunification, Douala Januari 27.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Charles Edward, Carlos Protas, Bakari Mwamnyeto Baraka Majogoro, Ayoub Lyanga/Adam Adam dk75, Feisal Salum, Yussuf Mhilu/Farid Mussa dk66, Lucas Kikoti/Deus Kaseke dk49 na Ditram Nchimbi.
  Zambia; Allan Chibwe, Benedict Chepeshi, Luka Banda, Clement Mwape, Zachariah Chilongoshi, Golden Mafwenta/ Spencer Sautu dk46, Paul Katema, Kelvin Kampamba/Amity Shamende dk68, Kelvin Kapumbu, Collins Sikombe na Emmanuel Chabula.
  REKODI YA NDAYIRAGIJJE TAIFA STARS
  1. Tanzania 0-0 Kenya (Kufuzu CHAN- Dar es Salaam)
  2. Tanzania 0-0 (penalti 4-1) Kenya (Kufuzu CHAN – Nairobi)
  3. Tanzania 1-1 Burundi (Kufuzu Kombe la Dunia – Bujumbura)
  4. Tanzania 1-1 (Penalti 3-0) Burundi (Kufuzu Kombe la Dunia – Taifa)
  5. Tanzania 0-1 Sudan (Kufuzu CHAN – Taifa)
  6. Tanzania 0-0 Rwanda (Kirafiki Kigali)
  7. Tanzania 2-1 Sudan (Kufuzu CHAN – Omdurman)
  8. Tanzania 2-1 Equatorial Guinea (Kufuzu AFCON – Taifa)
  9. Tanzania 1-2 Libya (Kufuzu AFCON Tunisia)
  10. Tanzania 0-1 Burundi (Kirafiki Taifa)
  11. Tanzania 0-1 Tunisia (Kufuzu AFCON Tunisia)
  12. Tanzania 1-1 Tunisia (Kufuzu AFCON Benjamin Mkapa)
  13. Tanzania 1-1 DRC (Kirafiki Benjamin Mkapa)
  14. Tanzania 0-2 Zambia (CHAN 2021 – Omdurman)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANZANIA YAANZA VIBAYA MICHUANO YA CHAN CAMEROON, YACHAPWA MABAO 2-0 NA ZAMBIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top