• HABARI MPYA

    Wednesday, January 13, 2021

    YANGA SC WATWAA KOMBE LA MAPINDUZI BAADA YA KUIFUNGA SIMBA KWA PENALTI 4-3 ZANZIBAR

    Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
    VIGOGO, Yanga SC wamefanikiwa kutwaa Kombe la Mapinduzi baada ya ushindi wa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 usiku wa leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar. 
    Shujaa wa Yanga SC kwenye mchezo wa leo ambao mgeni rasmi alikuwa Rais mpya wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi alikuwa ni kipa Farouk Shikaro aliyeokoa penalti ya mwisho ya Simba iliyopigwa na Mkenya mwenzake, beki Joash Onyango. 
    Penalti za Yanga SC leo zimefungwa na Mkongo Tuisila Kisinda, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Zawadi Mauya na Mrundi Said Ntibanzokiza, wakati Mkongo mwingine, Mukoko Tonombe iliokolewa na kip Beno Kakolanya wa Simba.


    Penalti za Simba SC zilifungwa na kiungo Mkenya Francis Kahata, mshambuliaji Mkongo Chriss Mugalu na beki mzawa Gardiel Michael, wakati mshambuliaji Mnyarwanda, Meddie Kagere na Nahodha wa leo, aligongesha mwamba wa juu kulia.
    Dakika 90 za mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nasor aliyesaidiwa na Mustafa Khamisi Hasira na Ali Ahmada Mbwana pembezoni mwa Uwanja, mezani Issa Haji Vuai na Kamisaa Muhidini Kamara zilikuwa tamu na za kusisimua miamba hiyo ikitoshana nguvu.
    Hii inakuwa mara ya pili kwa Yanga SC kutwaa Kombe la Mapinduzi baada ya mwaka 2007 mashindano hayo yalipofanyika kwa mara ya kwanza na wakaifunga Mtibwa Sugar kwenye fainali.  
    Lakini inakuwa mara ya kwanza kuwafunga watani wao hao wa jadi kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mara mbili awali – Januari 10, 2017 kwenye Nusu Fainali kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 na Januari 12, mwaka 2011 kwenye Fainali ilipochapwa 2-0, mabao ya Mussa Hassan Mgosi na Shijja Mkinna.
    Nyota watatu wa Simba walijinyakulia tuzo baada ya mchezo huo, Wakenya beki Joash Onyango Mchezaji Bora wa Mechi, Kiungo Francis Kahata Mchezaji wa Bora wa Mashindano na Mshambuliaji Miraj Athumani Mfungaji Bora kwa mabao yake manne.
    Mkenya mwingine, kipa Farouk Shikaro wa Yanga amejinyakulia tuzo ya Kipa Bora kufuatia kuruhusu bao moja tu kwenye mashindano haya.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Adeyoum Saleh/Paul Godfrey ‘Boxer’ dk71, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Said Juma ‘Makapu’, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Zawadi Mauya, Michael Sarpong/Waziri Junior dk83, Said Ntibanzokiza na Haruna Niyonzima.
    Simba SC; Beno Kakolanya, David Kameta, Gardiel Kameta, Kennedy Juma, Joash Onyango, Thadeo Lwanga, Hassan Dilunga/Chris Mugalu dk61, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Francis Kahata na Miraj Juma/Ibrahim Ajibu dk72.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WATWAA KOMBE LA MAPINDUZI BAADA YA KUIFUNGA SIMBA KWA PENALTI 4-3 ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top