• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 21, 2021

  MWAMBUSI AONDOKA TENA YANGA WIKI MOJA TU BAADA YA TIMU KUBEBA KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Msaidizi wa klabu ya Yanga, Juma Mwambusi amejiondoa kwa kile alichokieleza sababu za kiafya.
  Mwenyekiti wa klabu, Dk Mshindo Msolla amethibitisha kujiuzulu kwa Mwambusi aliyekuwa anafanya kazi kwa awamu ya pili Yanga baada ya awali kufanya kazi chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm na Mzambia, George Lwandamina.
  Msolla amesema kwamba watazungumza na kocha Mkuu, Mrundi Cedric Kaze kupata maoni yake juu ya msaidizi mpya amtakaye.


  Lakini tayari kuna tetesi kwamba kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Nizar Khalfan ndiye atakayechukua nafasi hiyo kwa sababu ndiye chaguo la Kaze.
  Wakati Kaze alikuwa anafundisha akademi ya Barcelona nchini Canada, Nizar Khalfan amechezea timu ya Vancouver Whitecaps ya nchini humo, ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
  Mwambusi ndiye kocha aliyekiandaa kikosi cha Yanga kwa ajili ya msimu huu kabla ya kuletwa Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyedumu kwa mwezi mmoja tu na kuondolewa akimpisha Kaze.
  Hata hivyo baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga ikiwa inaongoza na pia kubeba Kombe la Mapinduzi wiki iliyopita, Mwambusi anaondoka tena Jangwani. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWAMBUSI AONDOKA TENA YANGA WIKI MOJA TU BAADA YA TIMU KUBEBA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top