• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 26, 2021

  PULEV AWASILI NCHINI KUMSAPOTI MDOGO WAKE ANAPIGANA DAR

  BONDIA nyota wa uzito wa juu duniani, Mbulgaria Kubrat Pulev amewasili Dar es Salaam leo kumsaidia mdogo wake,Tervel Pulev ambaye Ijumaa atakuwa anapigana nchini.
  Kubrat aliyepigwa kwa Techunical Knockout (TKO) na Muingereza, Anthony Joshua mwishoni mwa kwaka jana alikuwa mwenye furaha wakati anawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam.
  Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesema kuwa itatumia mapambano ya 'Rumble in Dar' kuutangaza utalii wa nchi.
  Siku hiyo pambano kuu ni kati ya Mtanzania, Ibrahim Mgendera 'Ibrah Class' na Mmalawi anayeishi Afrika Kusini, Dennis Mwale kuwania taji la Mabara la WBF uzito wa Super Feather.
  Mapambano hayo yaliyoandaliwa na kampuni ya Jackson Group Sports yatafanyika ukumbi wa Next Door Arena, Masaki Jijini Dar es Salaam na kuonyeshwa nchi zaidi ya 150 duniani kupitia Azam Sports 1 HD.  
  Siku hiyo pia kutakuwa na mapambano mengine nane yalishirikisha mabondia mbalimbali ikiwa pamoja na Tervel Pulev atakayepigana na Vikapita Merero wa Namibia uzito wa Cruiser.
  Mkurugenzi wa Masoko wa TTB, Mindi Kasiga amesema leo kwamba watatumia fursa hiyo kuutangaza utalii wa nchi kwani mapambano ya ngumi hayo yataonekana nchi nyingi.
  “Hii ni fursa kwetu kuutangaza utalii na kuingia kusapoti Jackson Group Sports,” aliema Kasiga.
  Mbali ya TTB, pambano hilo limedhaminiwa na benki ya CRDB ambapo meneja wa chapa, Joe Bendera alisema kuwa wanazidi kuendeleza michezo nchini kwani walidhamini pia mpira wa kikapu, kuandaa marathoni na kutoa fursa ya masomo kwa vijana 26 kupitia mpira wa kikapu.
  Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Global Boxing Stars (GBS), Scott Farrell alisema kuwa wamevutiwa na kampuni ya Jackson Group Sports na kuamua kufanya nao kazi pamoja kuinua mhezo wa ngumi za kulipwa.
  Alisema kuwa  lengo lao ni kuinua vipaji vya mchezo huo hapa nchini. Mbali ya wadhamini hao, wadhamini wengine ni Azam TV, Onomo Hotel, Precision Air, Vitasa, Bono 5, Hotel Demag na Henessy.
  Mkurugenzi Mtendaji a Jackson Group Sports, Kelvin Twissa alisema kuwa maandalizi ya pambano hilo yamekamilika na mabondia wote wamewasili kwa ajili ya kuzichapa Ijumaa.
  Twissa alisema kuwa kila bondia ana ari kubwa ya kushinda katika pambano hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PULEV AWASILI NCHINI KUMSAPOTI MDOGO WAKE ANAPIGANA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top