// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); YANGA SC BADO HAWAJAONA UMUHIMU WA KUWAPIMA AFYA WACHEZAJI KABLA YA KUWASAJILI, AU? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE YANGA SC BADO HAWAJAONA UMUHIMU WA KUWAPIMA AFYA WACHEZAJI KABLA YA KUWASAJILI, AU? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, December 03, 2014

    YANGA SC BADO HAWAJAONA UMUHIMU WA KUWAPIMA AFYA WACHEZAJI KABLA YA KUWASAJILI, AU?

    SIMBA SC imeusogeza mbele Mkataba wa Mkenya, Paul Raphael Kiongera kutoka kuanza msimu huu kama ilivyotakiwa hadi msimu ujao.
    Hiyo inafuatia mchezaji huyo kuumia katika mechi ya kwanza tu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, dhidi ya Coastal Union ya Tanga Septemba 21, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Awali ya hapo, Kiongera alicheza mechi tatu za kirafiki na kufunga mabao mawili na Simba SC ilikiri mapema kumsajili mchezaji huyo akiwa majeruhi.
    Kiongera alitonesha goti lake katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zikitoka sare ya 2-2.

    Mkenya huyo aliingia kipindi cha pili, lakini dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho akatoka baada ya kuumia, kufuatia kugongana na kipa Shaaban Kado.
    Baaada ya hapo, Kiongera alikwenda kufanyiwa vipimo na kugundulika ameumia sana- hivyo kuhitaji mapumziko ya wiki sita, ambazo zimekwisha na hajapona.
    Simba SC sasa inaingia gharama za kumpeleka India kwa matibabu zaidi, ambayo yatamuweka nje kwa zaidi ya miezi mingine mitatu.
    Na bahati nzuri, wawili hao wametiliana saini makubaliano ya Mkataba kusogezwa mbele kutoka msimu huu hadi ujao.
    Hali kama hii iliwatokea Azam FC kwa kiungo Frank Domayo walimsajili kutoka Yanga SC akiwa majeruhi, hivyo wakaingia gharama za kumtibu na atakuwa nje hadi mapema mwakani.    
    Domayo naye hataitumikia Azam FC katika mwaka wake wa kwanza kwenye mkataba wake wa miaka miwili, lakini haijulikani makubaliano yake na klabu hiyo yako vipi.
    Ninakumbuka, mwaka 2004 Yanga SC ilimsajili mshambuliaji Patrick Kataray kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa pamoja na Pitchou Kongo.
    Kongo aliitumikia vizuri tu Yanga SC kwa misimu miwili, lakini Kataray alikuwa majeruhi na hakuwahi kuutumikia vizuri mkataba wake.
    Anacheza mechi mbili, mwezi mzima yuko nje anauguza nyama. 
    Haya yote ni matatizo ambayo yanaweza kuepukika, iwapo klabu itamfanyia vipimo mchezaji kabla ya kumsajili.
    Manchester United ilikuwa tayari kumsajili Mholanzi Ruud van Nisterlooy kwa dau la rekodi katika klabu hiyo wakati huo, Pauni Milioni 18.5 mwaka 2000, lakini ikataka afanyiwe vipimo vya kina kutokana na hofu ya maumivu yake ya goti.
    Lakini United iliamua kuachana na mchezaji huyo, baada ya klabu yake wakati huo, PSV Eindhovein kukataa mshambuliaji huyo kufanyiwa vipimo vya kina na siku moja baada ya kukataa, Van Nisterlooy akaumia goti lililomuweka nje kwa mwaka mzima.
    Lakini mwaka mmoja, baadaye United ilimnunua mchezaji huyo kwa Pauni Milioni 19 na akaichezea timu hiyo hadi mwaka 2006 alipotimkia Real Madrid.
    United pia ilimsajili kwa mkopo mshambuliaji Radamel Falcao katika siku ya mwisho ya kufunga pazia la usajili msimu huu, ikisema kwamba kama hataendelea kusumbuliwa na tatizo la majeruhi, watamnunua moja kwa moja baadaye.
    Vipimo vya afya ni jambo muhimu- hata kama klabu imempenda mchezaji na kuamua kumsajili akiwa na maumivu, lakini aina ya Mkataba itakuwa tofauti.
    Watu wananunua magari yenye dosari, lakini kwa utashi wao na kwa bei ambazo zinaendana na magari yenyewe, wakijua kabisa wataingia gharama za marekebisho.
    Tumeona, kwa makosa ambayo Simba SC walifanya awali kwa Kiongera hawajataka kuyarudia wakati wanamsajili Mganda, Dan Sserunkuma.
    Simba SC walimfanyia vipimo vya afya mchezaji huyo kabla ya kumpa Mkataba wa miaka miwili, ingawa ametoka Gor Mahia akiwa anacheza kwa kiwango cha juu, kiasi cha kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu.
    Na Azam FC pia, baada ya kuingia mkenge kwa Domayo, hawakutaka kurudia makosa hayo kwa beki Serge Wawa Pascal, raia wa Ivory Coast aliyekuwa anachezea El Merreikh ya Sudan.
    Pamoja na kwamba walikutana na Wawa akiwa na Merreikh mjini Kigali, Rwanda katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati Agosti mwaka huu, lakini walilazimika kumfanyia vipimo vya afya kabla ya kumsajili.
    Lakini ajabu tu ni kwamba, Yanga SC wameleta mchezaji kutoka Brazil, Emerson de Oliveira Roque ambaye baada ya majaribio ya siku tatu, akapewa Mkataba wa mwaka mmoja.
    Tovuti ya Yanga SC ilichapisha picha ya mchezaji huyo anasaini Mkataba tu- lakini haikuwa na picha ya anafanyiwa vipimo vya afya na wala haikuvuja popote, iwe kwenye mitandao au vyombo vingine vya habari.  
    Labda, inawezekana Yanga walimfanyia vipimo Emerson, lakini hawakuona umuhimu wa kuzitoa hadharani. Kama ni hivyo sawa, ila kama zoezi hilo halikufanyika watakuwa wamefanya makosa.
    Sitaki kujua kama majaribio aliyoyafanya yalitosha kujiridhisha kumpa Mkataba, au la- isipokuwa tu nitastaajabu sana kama Yanga SC hadi leo hawajaona umuhimu wa kuwapima wachezaji afya kabla ya kuwasajili. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC BADO HAWAJAONA UMUHIMU WA KUWAPIMA AFYA WACHEZAJI KABLA YA KUWASAJILI, AU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top