• HABARI MPYA

  Friday, September 10, 2021

  ZACHARIA HANS POPPE AFARIKI DUNIA

  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amefariki dunia usiku huu katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
  Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Aldo Hans Poppe msiba upo nyumbani kwake, Ununio Jijini Dar es Salaam na taarifa zaidi zitatolewa kesho baada ya kikao cha kifamilia.
  Zacharia Hans Poppe alizaliwa Oktoba 15, mwaka 1956 mjini Dar es Salaam na kukulia mkoani Iringa.
  Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, Zacharia alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza, ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1983.


  Lakini mwaka 1995, Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William Mkapa, rais wa awamu ya tatu.
  Kama zinavyosema sheria za nchi, mtu aliyehukumiwa kifungo, hana haki ya kugombea wadhifa wowote au kuajiriwa tena, Zacharia naye hakuweza kurejea kazini, badala yake akaamua kujiajiri, kwa kuanzisha miradi yake mwenyewe, ikiwemo kampuni ya usafirishaji ZH Poppe.
  Amekuwa mpenzi wa Simba SC tangu miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe aliwahi kusema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi, walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.
  Amekuwa Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji tangu mwaka 2010 na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili tangu 2012 kabla ya kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi katika mfumo mpya wa uendeshwaji klabu tangu mwaka jana.
  MUNGU AMPUMZISHE KWA AMANI.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZACHARIA HANS POPPE AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top