• HABARI MPYA

    Sunday, September 12, 2021

    HANS POPPE KUAGWA KESHO KARIMJEE HALL

    MWILI wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe aliyefariki dunia juzi jioni hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salam utaagwa kesho kuanzia Saa 3:00 asubuhi ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
    Taarifa iliyotlewa na klabu ya Simba leo imesema kwamba mwili wa marehemu Zacharia Hans Poppe utasafirihwa Jumanne kwenda kwao Iringa kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumatano makaburi ya familia, Kihesa, Mkimbizi mkoani humo.
    Zacharia Hans Poppe alizaliwa mwaka 1956 mjini Dar es Salaam na kukulia mkoani Iringa na baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambako alifikia cheo cha Kapteni, kabla ya kuachishwa kazi na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, kwa tuhuma za uhaini, dhidi ya serikali ya awamu ya kwanza, ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwaka 1983.


    Lakini mwaka 1995, Zacharia aliachiwa huru kwa msamaha wa rais wa awamu ya pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, mwezi mmoja kabla hajamuachia Ikulu ya Tanzania, Benjamin William Mkapa, rais wa awamu ya tatu na baada ya hapo akajiajiri kwa kuanzisha kampuni ya usafirishaji ZH Poppe ambayo imekuwa kubwa barani.
    Amekuwa mpenzi wa Simba SC tangu miaka ya 1970, akiwa kijana mdogo na zaidi mwenyewe aliwahi kusema, mechi ambayo ilimfanya ajitamke rasmi yeye ni Simba damu ilikuwa dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga Juni 23, mwaka 1973, ambayo Wekundu wa Msimbazi, walishinda 1-0, bao pekee la Haidari Abeid ‘Muchacho’ dakika ya 68.
    Amekuwa Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji tangu mwaka 2010 na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili tangu 2012 kabla ya kuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi katika mfumo mpya wa uendeshwaji klabu tangu mwaka jana. RIP Hans Poppe.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE KUAGWA KESHO KARIMJEE HALL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top