• HABARI MPYA

  Monday, December 01, 2014

  SSERUNKUMA KUTUA JUMATANO KUMWAGA WINO SIMBA SC, KIONGERA AENDA INDIA KESHO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mkenya, Paul Kiongera anaondoka kesho Dar es Salaam kwenda India kwa matibabu, lakini klabu yake Simba SC imemuondoa kwenye orodha ya wachezaji watakaocheza sehemu iliyobaki ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mfungaji bora wa Kenya kwa misimu miwili iliyopita, Daniel Sserunkuma atarejea Dar es Salaam Jumatano kusaini Mkataba wa mwaka mmoja baada ya mazungumzo yaliyopata mwafaka wiki iliyopita.
  Na mshambuliaji huyo wa Gor Mahia ya Kenya ndiye atakayechukua nafasi ya Mkenya, Kiongera ambao waliwahi kucheza pamoja klabu hiyo ya Nairobi chini ya kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic.
  Dan Sserunkuma anakuja Jumatano kusaini Mkataba Simba SC

  Lakini wachezaji wengine kutoka nchi za Magharibi mwa Afrika wanakuja kufanya majaribio Simba SC  na iwapo wataonekana wanafaa, kuna hatari ya wachezaji wa kigeni waliopo sasa kwenye kikosi cha timu hiyo kutemwa.
  Mbali na Kiongera, wageni wengine kikosini Simba SC ni Waganda beki Joseph Owino na mshambuliaji Emanuel Okwi na Warundi, kiungo Pierre Kwizera na mshambuliaji Amisi Tambwe.
  Kwa kuwa baada ya kufanyiwa upasuaji India, Kiongera atahitaji si chini ya miezi mitatu ya mapumziko, maana yake atarejea Ligi Kuu ikiwa imefika ukingoni, Simba SC imeona bora imuondoe katika usajili.
  Kiongera aliifungia Simba SC mabao mawili kwenye mechi tatu kabla ya kuumia katika mechi ya nne

  Lakini Simba SC haina kabisa mpango wa kumtema Kiongera, zaidi ya kumtibu apone ili baadaye aje kuitumikia klabu- isipokuwa Mkataba wake utasogezwa mbele kwa maana ya kipindi cha matibabu kutohesabiwa kama alikuwa kazini.
  Simba SC ilimsajili Kiongera akiwa majeruhi kutoka Kenya na kwa bahati mbaya akatonesha goti lake katika mchezo wa kwanza tu wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union.
  Awali, mchezaji huyo mrefu alicheza mechi tatu za kirafiki na kufunga mabao mawili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SSERUNKUMA KUTUA JUMATANO KUMWAGA WINO SIMBA SC, KIONGERA AENDA INDIA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top