• HABARI MPYA

  Wednesday, September 01, 2021

  MBWANA SAMATTA AREJEA UBELGIJI KWA MKOPO

  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Samatta amejiunga na Royal Antwerp ya Ubelgiji kwa mkopo kutoka Fenerbahçe ya Uturuki ambayo nayo ilimchukua kwa mkopo Aston Villa.
  Samatta mwenye umri wa miaka 28 anarejea Ubelgiji, nchi yake ya kwanza ya Ulaya kucheza kabla ya kwenda England na baadaye Uturuki.
  Samatta anaondoka Fenerbahçe baada ya kucheza jumla ya mechi 30 na kufunga mabao mabao matano tu kufuatia kutua Uturuki kwa mkopo wa hadi mwishoni mwa msimu alipouzwa moja kwa moja kwa ada ya Pauni Milioni 5.5 kumalizia mkataba wake wa Villa.
  Samatta alijiunga na Aston Villa Januari mwaka jana kwa dau la Pauni Milioni 10 kutoka klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.


  Villa alicheza mech 14 tu hadi sasa na kufunga mabao mawili – Aston Villa ikichapwa 2-1 na wenyeji, AFC Bournemouth mechi ya Ligi Kuu alifunga kwa kichwa dakika ya 70 Uwanja wa Vitality.
  Siku hiyo AFC Bournemouth iliyomaliza pungufu baada ya Jefferson Lerma kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 51, ilitangulia kwa mabao ya kiungo wa kimataifa wa Denmark, Philip Billing dakika ya 37 na beki Mholanzi, Nathan Ake dakika ya 44.
  Samatta akafunga tena bao la kufutia machozi Aston Villa ikichapwa 2-1 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi England Uwanja wa Wembley Jijini London.
  Manchester City inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pep Guardiola ilitangulia kwa mabao ya mshambuliaji wake tegemeo, Muargentina Sergio Aguero dakika ya 20 akimalizia pasi ya Philip Foden na Rodri Hernandez akimalizia pasi ya İlkay Gundogan dakika ya 30.
  Samatta aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016. 
  Akiwa Genk, Samatta ambaye sasa ndiye Nahodha wa Taifa Stars, alifunga mabao 76 katika mechi 191 hadi Aston Villa kuvutiwa naye na kumnunua.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBWANA SAMATTA AREJEA UBELGIJI KWA MKOPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top