• HABARI MPYA

  Saturday, July 03, 2021

  YANGA SC WAWANYAMAZISHA SIMBA SC MBELE YA RAIS MAMA SAMIAH, WAICHAPA 1-0 BAO PEKEE LA ZAWADI MAUYA

  VIGOGO, Yanga SC wamezima kelele za watani wao wa jadi, Simba SC baada ya kuwachapa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, Yanga SC inafikisha pointi 70 katika mchezo wa 31, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi tatu na mabingwa hao watetezi kwa kwa misimu sasa, Simba SC ambao pia wana mechi mbili mkononi.
  Ikumbukwe Simba ilihitaji sare tu kutawazwa rasmi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa nne mfululizo na sasa watalazimika kusubiri hadi mechi ijayo baada ya watani kukataa kuwa ngazi ya ubingwa wao mwingine. 
  Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, bao pekee la Yanga limefungwa na kiungo Zawadi Mauya dakika ya 11 kwa shuti la umbali wa mita 21 baada ya kupokea pasi ya kiufundi ya kiungo mwenzake, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
  Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa kwenye kona fupi ambayo Deus Kaseke alimuanzishia Mkongo Tuisila Kisinda akamrudhishia na kupiga krosi iliyopanguliwa na kipa Aishi Manula, mpira ukamkuta Feisal akiwa amebanwa na walinzi wa Simba akatoa pasi ya nyuma kwa Mauya aliyefumua shuti la bao. 
  Katika mchezo huo wachezaji wanne wa Yanga walionyeshwa kadi za njano, kipa Faruk Shikalo, beki Adeyum Ahmed na viungo Mkongo Mukoko Tonombe na Feisal Salum, wakati kwa Simba ni mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Mkenya Joash Onyango pekee walioonywa kwa adhabu hiyo.
  Huo ulikuwa mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu baada ya ule wa Novemba 7, mwaka jana kumalizika kwa sare ya 1-1 hapo hapo Benjamin Mkapa, Yanga SC wakitangulia kwa bao la penalti la mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kipindi cha kwanza, kabla ya beki Mkenya Joash Onyango kuisawazishia Simba mwishoni mwa kipindi cha pili.
  Kipigo cha leo kinakumbushia machungu ya kichapo cha Machi 8, mwaka jana 1-0 pia hapo hapo Benjamin Mkapa bao pekee la Mghana ambaye sasa amehamia Simba, Bernard Morrison dakika ya 44, mchezo ambao ulihudhuriwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Dk John Pombe Magufuli.
  Kwa mwaka huu, Yanga imeipa kipigo cha pili Simba pamoja na ushindi wa Januari 13 wa penalti 4-3 kufuatia sare ya 0-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Na vigogo hao watakutana tena Julai 23 Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma katika Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joash Onyango, Serge Wawa, Thadeo Lwanga/Kope Mutshimba Mugalu dk82, Bernard Morrison, Erasto Nyoni/ Rally Bwalya dk46, John Bocco, Clatous Chama/Medie Kagere dk68 na Luis Miquissone. 
  Yanga SC; Farouk Shikharo, Kibwana Shomari, Adeyoum Ahmed, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda/Saido Ntibanzokiza dk87, Zawadi Mauya, Yacouba Sogne, Feisal Salum/ Said Juma ‘Makapu’ dk85 na Deus Kaseke/ Ditram Nchimbi dk72.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WAWANYAMAZISHA SIMBA SC MBELE YA RAIS MAMA SAMIAH, WAICHAPA 1-0 BAO PEKEE LA ZAWADI MAUYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top