• HABARI MPYA

    Sunday, July 25, 2021

    MWENYEKITI WA ZAMANI WA TFF, ALHAJ SAID HAMAD EL MAAMRY AFARIKI DUNIA AKIWA ANA UMRI WA MIAKA 86.

    MWENYEKITI wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho (TFF) na aliyekuwa Kamishna wa Jeshi la Polisi nchini, Wakili Said Hamad El Maamry amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jijini Dar es Salaam akiwa ana umri wa miaka 86. 
    Alhaj El Maamry amefariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kiharusi kwa zaidi ya miaka mitano, yaliyomsababishia maradhi ya kifua, shingo na mkono wa kulia kushindwa kufanya kazi kwa kipindi chote hicho.
    El Maamry ambaye mwaka 1973 kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa FAT katika uchaguzi mkuu uliofanyika Tanga, amewahi kuwa mjumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuanzia mwaka 1980 hadi 1986 kabla ya kuteuliwa kuwa Mjumbe wa heshima mwaka 1998.


    El Maamry ambaye akiwa kiongozi mkuu wa soka ya Tanzania, Taifa Stars ilicheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza mwaka 1980, amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
    Mwaka 1976 Waziri wa Michezo, Mirisho Sarakikya alivunja Kamati ya Utendaji ya FAT iliyoongozwa na El Maamry kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utawala mbovu, akambakisha madarakani Katibu Mkuu, Hassan Chabanga Dyamwalle pekee (marehemu pia).
    Hayo yalifanyika wakati Taifa Stars ikiwa na mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Nigeria kujiandaa na mechi za kufuzu kucheza Fainali za Afrika ambazo zilikuwa zikifanyika Addis Ababa Ethiopia ndipo El Maamry akaambiwa kuanzia siku ile si Mwenyekiti tena wa FAT lakini aendelee kuwa karibu na wageni mpaka watakapoondoka.
    Hata hivyo, serikali ikamruhusu kugombea katika uchaguzi wa FAT uliofanyika mwaka huo huo na akashinda na kuendelea kuongoza hadi mwaka 1986 alipoondoshwa akiwa kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Mexico ambako alialikwa, kabla ya kupigwa marufuku hata kugombea aliporejea kufuatia mchujo wa wagombea kufanywa akiwa nje ya nchi.
    Katika uchaguzi mkuu wa FAT uliofanyika Mbeya, nafasi ya Mwenyekiti hakupatikana mtu, hivyo Makamu Mwenyekiti Mbeyela akakaimu nafasi ya Mwenyekiti hadi mwaka 1989 alipochaguliwa Mohamed Mussa kuwa Mwenyekiti aliyeongoza FAT hadi mwaka 1992 huku El Maamry akibaki kuwa Mjumbe wa Heshima wa CAF tangu alipoteuliwa mwaka 1998.
    Mungu ampumzishe kwa amani. Amin.


    Marehemu Said El Maamry (kulia), hapa akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Morogoro akimshuhudia Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Lawi Nangwanda Sijaona akikagua timu ya soka ya Jeshi la Polisi Morogoro mwaka 1965.  


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWENYEKITI WA ZAMANI WA TFF, ALHAJ SAID HAMAD EL MAAMRY AFARIKI DUNIA AKIWA ANA UMRI WA MIAKA 86. Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top