• HABARI MPYA

  Sunday, July 18, 2021

  SIMBA SC WAKABIDHIWA KOMBE LA UBINGWA WA NNE MFULULIZO LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA NAMUNG0 FC 4-0

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WENYEJI, Simba SC wamekabidhiwa Kombe lao la nne mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi katika mchezo wa mwisho wa msimu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Simba SC leo yamefungwa na washambuliaji, Mnyarwanda Meddie Kagere dakika ya 19, Mkongo Kope Mutshimba Mugalu dakika ya 25 na 67 na mzawa, Nahodha John Raphael Bocco kwa penalti dakika ya 90 na ushei.
  Simba SC inamaliza msimu na pointi 83, tisa zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC ambao wamemaliza msimu kwa sare ya 0-0 na wenyeji, Dodoma Jiji Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

  Azam FC imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zao 68 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Ruvu Shooting bao pekee la kiungo Mudathir Yahya Abbas dakika ya 42 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  Pamoja na kufungwa 4-0 na wenyeji, Mbeya City mabao ya Siraji Juma dakika ya 10 na Juma Luizio matatu dakika ya 25, 46 na 49 Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya – lakini Biashara United imemaliza nafasi ya nne kwa pointi zake 50.
  KMC imemaliza nafasi ya tano kwa pointi zake 48 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Ihefu SC bao pekee la Charles Ilanfya dakika ya 81 Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Polisi Tanzania imemaliza nafasi ya sita kwa pointi zake 45 baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC bao pekee la Jimmy Shoji dakika ya 48 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
  Tanzania Prisons imemaliza nafasi ya saba kwa pointi zake 44 baada ya sare ya 1-1 Gwambina Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, wakati Dodoma Jiji iliyoa 0-0 na Yanga leo imemaliza nafasi ya nane kwa pointi zake 44 pia.
  Baada ya kuchapwa 4-0 na Simba leo, Namungo FC imemaliza nafasi ya tisa kwa pointi zake 43, wakati Mbeya City imemaliza nafasi ya 10 kwa pointi zake 42, Ruvu Shooting nafasi ya 11 pointi 41 na Kagera Sugar imekamilisha timu 12 zitakazoendelea na Ligi Kuu msimu ujao kwa pointi zake 40.
  Baada ya kuchapwa 2-1 na JKT Tanzania leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam, na kumaliza na pointi 39, Mtibwa Sugar itakwenda kumenyana na Transit Camp ya Daraja la Kwanza kuwania kubaki Ligi Kuu. 
  Nayo Coastal Union iliyoshinda 3-1 dhidi ya Kagera Sugar leo Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga na kumaliza na pointi 40 itakwenda kumenyana na Pamba FC ya Mwanza kuwania kubaki Ligi Kuu.
  JKT iliyomaliza na pointi 39, Gwambina FC 35 sawa na Ihefu – zote tatu zimeungana na Mwadui FC iliyoshika mkia kwa pointi zake 19 kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAKABIDHIWA KOMBE LA UBINGWA WA NNE MFULULIZO LIGI KUU BAADA YA KUICHAPA NAMUNG0 FC 4-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top