• HABARI MPYA

  Tuesday, November 07, 2023

  FEISAL SALUM AREJESHWA TAIFA STARS KUFUZU KOMBE LA DUNIA  KOCHA Mualgeria, Adel Amrouche amemrejesha kiungo Feisal Salum Abdallah kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania kitakachoingia kambini wiki hii kwa ajili ya mechi za Kundi E kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Niger na Morocco.
  Taifa Stars watakuwa wageni wa Niger Novemba 18, Uwanja Marrakech nchini Morocco, kabla ya kuwakaribisha Morocco Novemba 21, mwaka huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Taifa Stars imepangwa Kundi E pamoja na Kongo, Eritrea, Morocco, Niger na Zambia kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 zinazoandaliwa kwa pamoja na nchi za Canada, Mexico na Marekani.
  Timu tisa zitakazoongoza makundi zitafuzu moja kwa moja kuiwakilisha kwenye Fainali za Kombe la Dunia, wakati washindi wa pili bora wanne wa makundi watamenyana katika Nusu Fainali na Fainali na mshindi atakwenda kushiriki mchujo wa Mabara kuwania nafasi ya kwenda Kombe la Dunia pia.
  Mchujo wa Mabara, unaojulikana kama Inter-Confederation Play-Offs ni michuano mingine midogo inayoshirikisha timu sita za Mabara manne duniani, kasoro UEFA pamoja na nchi mwenyeji kutoka CONCACAF kutafuta timu mbili za mwisho za kushiriki michuano hiyo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FEISAL SALUM AREJESHWA TAIFA STARS KUFUZU KOMBE LA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top